Na.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Iringa
Serikali itaendelea kuwawezesha vijana kwa
kuwatengenezea mazingira mazuri ya mikopo ili waweze kujiajiri kupitia viwanda.
Kauli hiyo ilitolewa na mkuu wa mkoa wa Iringa,
Amina Masenza katika hotuba yake ya uzinduzi wa kongamano la kuhamasisha vijana
kushiriki ujenzi wa Tanzania ya viwanda lililofanyika katika ukumbi wa Siasa ni
Kilimo mjini Iringa jana.
Masenza alisema kuwa serikali inatambua umuhimu wa
vijana na imetengeneza mazingira mazuri ya uwezeshaji mikopo yenye riba nafuu
kwa vijana. Alisema kuwa uwezeshaji huo hufanyika kupitia mifuko mbalimbali
ukiwemo, mfuko wa maendeleo ya vijana ambao upo halmashauri na mfuko wa wajasiriamali
ambao upo SIDO.
“Hivyo, nitoe rai kuwa mifuko hii itakuwa ni kichocheo na
chanzo mojawapo ya mitaji kwa vijana ya kuanzishia viwanda Vidogo” alisema
Masenza.
Akiongelea uwekezaji katika sekta ya kilimo na
mifugo, mkuu wa mkoa alisema kuwa mkoa una hali nzuri ya hewa inayoruhusu
ustawi wa mazao ya aina mbalimbali ya chakula na biashara. Alisema kuwa mkoa
una fursa za uwekezaji katika viwanda vya usindikaji wa matunda, mbogamboga,
mazao ya nafaka na mafuta.
Vingine ni viwanda vya kusindika maziwa, nyama na
vyakula vya mifugo. Uwekezaji mwingine aliutaja kuwa katika viwanda vya
kutengeneza zana za kilimo kama mashine za kuvunia mazao ya mpunga, mahindi na
kupukuchua mahindi.
Kongamano la kuhamasisha vijana
kujiingiza katika shughuli za uzalishaji katika sekta viwanda na biashara na
uzinduzi wa kampeni yenye kaulimbiu ya ‘kijana hamasika, shiriki kikamilifu
kuiunda Tanzania ya viwanda’.
=30=