Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Iringa
Serikali
mkoani Iringa imewataka wakandarasi wa ujenzi wa miradi ya barabara kujipanga
sawasawa katika kutekeleza miradi ya ujenzi ili idumu kwa muda mrefu.
Kauli
hiyo ilitolewa na mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza katika hotuba yake ya
halfa ya utiaji saini mikataba baina ya TARURA na wakandarasi katika ukumbi wa
mikutano wa ofisi ya mkuu wa Mkoa jana.
Masenza
aliwataka wakandarasi wote walioshinda zabuni za ujenzi wa barabara katika Mkoa
wa Iringa kujipanga sawasawa. “Serikali
imewekeza pesa nyingi katika ujenzi wa barabara kwa lengo la kujenga na
kuimarisha barabara ili mwananchi aweze kunufaika na barabara hizo. Tumesikia
katika taarifa ya mratibu wa TARURA Mkoa wa Iringa kuwa gharama za ujenzi wa barabara
ni shilingi bilioni 3.56” alisema Masenza.
Aidha, alitumia hafla hiyo
kuwataka wakandarasi wote kufanya kazi kwa kuzingatia muda uliopangwa na
viwango vya ubora wa kazi. Serikali haitamvumilia mkandarasi yeyote
atakayefanya kazi chini ya muda uliopangwa kwenye mkataba wala kazi iliyofanywa
chini ya kiwango, aliongeza Masenza.
Katika
kuhakikisha ubora wa kazi za ujenzi, mkuu wa mkoa wa Iringa aliwataka mameneja
wa TARURA wa halmashauri kuwasimamia wakandarasi ili watekeleze majukumu yao. “Serikali imeajiri mameneja wa TARURA katika
halmashauri. Jukumu kubwa la mameneja hawa ni kuwasimamia wakandarasi ili
watekeleze wajibu wao. Hivyo, mameneja wa halmashauri pia mjipange sawasawa
kuhakikisha ubora na thamani ya fedha inapatikana” alisisitiza mkuu wa mkoa.
Mkuu
wa mkoa alitoa wito wa kulipwa kwa wakati pindi wakandarasi watakapotimiza
wajibu wao kwa kuzingatia vigezo vya ubora kwa mujibu wa mikataba iliyosainiwa.
Alisema kuwa kuna wakati malipo ya wakandarasi yamekuwa yakicheleweshwa
kutokana na uzembe na kutofuata taratibu. “Utekelezaji
huo utawafanya kuongeza morari ya kazi na pia kuondoa malalamiko yasiyo ya
lazima kwa Serikali” alisema mkuu wa mkoa.
Awali
mratibu wa TARURA Mkoa wa Iringa, mhandisi Juma Wambura katika taarifa yake
alisema kuwa TARURA Mkoa wa Iringa ilitangaza miradi ya barabara za halmashauri
zote za Mkoa jumla ya zabuni 26 zenye thamani ya shilingi bilioni 6.5. “Leo utaishuhudia mikataba 18 ikisainiwa na
wazabuni walioshinda baada ya mchakato mzima wa manunuzi kukamilika yenye
thamani ya shilingi bilioni 3.56. Mhe. mkuu wa mkoa, mikataba takribani 8
itasainiwa baadae baada ya taratibu za manunuzi kukamilika” alisema
mhandisi Wambura.
Mratibu
huyo alisema kuwa lengo la TARURA ni kufanikisha dhima kuu ya Serikali kuwa miundombinu
ya barabara inaboreshwa na kusonga mbele kwa mujibu wa sheria na taratibu za
nchi ili iweze kuboresha uchumi wa wananchi.
TARURA
mkoa wa Iringa inahudumia mtandao wa barabara wenye jumla ya Kilomita 4,601.25
inayojumuisha halmashuri tano za Manispaa, halmashauri za wilaya za Iringa,
Kilolo, Mufindi na Mji wa Mafinga.
=30=
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni