Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
ASILIMIA kubwa ya wanawake wa
Tanzania ni wahanga wa saratani ya mlango wa kizazi ikichangia vifo vingi
kutokana na wagonjwa wanaogundulika na ugonjwa huu wakiwa katika hatua
isiyotibika.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu Tawala
Mkoa wa Iringa, Wamoja Ayubu alipokuwa akizindua mradi wa kuhamasisha jamii
kuhusu huduma za uchunguzi wa saratani ya shingo ya kizazi uliofanyika katika
ukumbi wa chuo cha Veta mjini Iringa.
Amesema “Tanzania ni mojawapo ya nchi
zinazokumbwa na mzigo mkubwa wa saratani ya shingo ya kizazi duniani. Asilimia
25% ya wanawake wa Tanzania wako hatarini kupata saratani ya mlango wa kizazi
katika maisha yao, saratani hii ni mojawapo ya sababu kubwa zinazosababisha
vifo vya wanawake nchini”. Amesema kuwa asilimia 80 ya wagonjwa wanaogundulika
na aina hiyo ya saratani hugundulika katika hatua kubwa ya ugonjwa ambapo
hakuna tiba wala kinga.
Akiongelea takwimu kutoka taasisi ya
saratani ya Ocean road, amesema kuwa takwimu hizo zinaonesha kuwa kati ya
wagonjwa wa saratani wanaopelekwa katika taasisi hiyo kila mwaka, zaidi ya
wagonjwa 5,000 wana tatizo la saratani ya mlango wa kikazi. Amesema kuwa
serikali kupitia wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii inafanya juhudi mbalimbali
katika kupambana na saratani ya mlango wa kizazi kwa wanawake. Amesema kuwa
saratani ya mlango wa kizazi inatibika pale inapogundulika katika hatua za
awali.
Katibu Tawala Mkoa wa Iringa amesema
kuwa upo uhusiano mkubwa kati ya saratani ya mlango wa kizazi na maambukizi ya
virusi vya Ukimwi. Amesema kuwa takwimu za utafiti wa viashiria vya Ukimwi na
Malaria nchini zinaonesha kuwa na kiwango kikubwa cha maambukizi ya virusi vya
Ukimwi kwa asilimia 9. Amesema kuwa takwimu hiyo inatoa picha ya ukubwa wa
tatizo la saratani ya mlango wa kizazi kwa mkoa wa Iringa. Amesema kuwa
kutokana na ukubwa wa tatizo hilo, wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii peke yake
haiwezi kutatua tatizo la saratani ya mlango wa kizazi. Ametoa wito kwa wadau
mbalimbali kuunga mkono ili kuhakikisha kuwa akina mama na kina dada wako
salama dhidi ya tatizo hilo.
Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Wamoja Ayubu (kulia) na Mkurugenzi Mtendaji wa T-MARC TANZANIA Diana Kisaka |
Aidha, ametoa wito kwa wanawake na
wasichana kujitokeza kwa wingi ili kufaidika na huduma za uchunguzi wa awali
zitakazotolewa katika vituo mbalimbali vya afya mkoani Iringa. Vilevile, amewataka
wanaume kuwahamasisha akina mama na mabinti ili waweze kujitokeza kwa wingi
kupatiwa elimu na huduma ya uchunguzi itakayotolewa bure.
=30=
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni