Ijumaa, 25 Julai 2014

MAAFISA HABARI DUMISHENI USHIRIKIANO



Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Maafisa habari wa mkoa wa Iringa wametakiwa kudumisha ushirikiano wao ili kurahisisha ubadilishanaji wa habari kwa lengo la kuwafikishia huduma hiyo wananchi.
Kauli hiyo imetolewa na kaimu Katibu Tawala Msaidizi, Sehemu ya Utawala na Rasilimali watu, Neema Mwaipopo alipokuwa akifungua kikao kazi baina ya afisa habari wa mkoa wa Iringa na maafisa habari wa halmashauri nne za mkoa wa Iringa kilichofanyika katika ofisi ya mkuu wa Mkoa wa Iringa. 
Kaimu Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Utawala na Rasilimali watu, Neema Mwaipopo
Mwaipopo amesema “napenda niongelee suala la ushirikiano baina yenu katika kutekeleza majukumu yenu ya kihabari na majukumu mengine ya kiserikali”. Amesema kuwa mafanikio na ufanisi katika kazi hutegemea sana ushirikiano madhubuti baina ya wadau wa sekta husika. Ameongeza kuwa utaratibu mzuri wa kubadilishana habari na taarifa kwa mujibu wa taratibu za serikali kutasaidia kuleta chachu na ufanisi katika kazi za maafisa habari wa mkoa wa Iringa. Amesema kuwa kulegalega kwa ushirikiano baina ya maafisa habari kunachangia kudorora kwa ufanisi wa kazi katika tasnia ya habari.
Kaimu Katibu Tawala Msaidizi, Utawala na Rasilimali watu amesisitiza ushirikiano baina ya maafisa habari na vyombo vya habari. Amesema kuwa ushirikiano huo ni nyenzo muhimu katika kutekeleza majukumu ya maafisa habari. Amewataka kuendeleza na kuimarisha ushirikiano na vyombo vya habari vya mkoa wa Iringa. Aidha, amewataka kuvipatia msaada wa kitaalamu na kiufundi ili viweze kufanya kazi kwa weledi zaidi. Aidha, amewataka kuwa makini katika jukumu hilo kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu za serikali zilizopo.
Mwaipopo amesema “ni ukweli usio na shaka kuwa maafisa habari wana jukumu kubwa sana katika kuwapasha habari wananchi wa mkoani Iringa na Tanzania kwa ujumla kuhusu utendaji kazi wa serikali hasa utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya chama cha Mapindizi ya mwaka 2010”. Amesema kuwa maafisa hao wana jukumu la kutoa habari au kutengeneza mazingira ya kupatikana habari zinazoelezea fursa zilizopo katika maeneo yao zinazohusu uwekezaji”. Aidha, amewataka kuhakikisha serikali inasikika na shuguli zake zinafahamika kwa wananchi mkoani Iringa.
Mkuu huyo wa utawala amewataka maafisa habari kuhakikisha wanakamilisha mipango kazi yao ya mwaka ili waweze kutekeleza majukumu waliyojipangia kwa mwaka. Amesema “mpango kazi wa mwaka ni muongozo katika utekelezaji wa majukumu ya kila siku. Ni matumaini yangu kikao kazi hiki kitaweka azimio la kila afisa habari kutengeneza mpango kazi wake utakaokuwa dira katika utendaji kazi wake”. Vilevile, amewataka kuhakikisha wanakamilisha ujazaji wa fomu za mfumo wa upimaji wa wazi utendaji kazi (OPRAS). Amesema “niongelee kidogo umuhimu wa utekelezaji wa mfumo wa upimaji wa wazi wa utendaji kazi (OPRAS) kwa maafisa habari. Mfumo huu wa OPRAS umeanzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Utumishi wa Umma Na. 8 ya Mwaka 2002 kama ilivyorekebishwa na Sheria Na. 18 ya Mwaka 2007”. Amesema kuwa utekelezaji wake umesisitizwa katika Kanuni za Kudumu za Utumishi wa Umma toleo la Mwaka 2009 na kufafanuliwa zaidi katika Waraka wa Utumishi wa Umma Na. 2 wa Mwaka 2004. Amesitiza kuwa utaratibu huo maana yake kupanda cheo kwa afisa habari kutazingatia taarifa za upimaji wa wazi wa utendaji kazi (OPRAS).
Akiongelea lengo la kuandaa kikao kazi hicho baina ya afisa habari mkoa wa Iringa na maafisa habari wa halmashauri, afisa habari mkoa, Dennis Gondwe amesema kuwa kikao kazi hicho kimelenga kudumisha na kuimarisha ushirikiano baina ya maafisa habari hao. Amesmea kuwa kikao hicho linataka maafisa habari wawe na uelewa wa pamoja katika sekta ya habari na kuongeza wigo wa upatikanaji wa habari katika ofisi za umma.
Kaimu Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Utawala na Rasilimali watu katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Neema Mwaipopo (watatu kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Afisa Habari Mkoa na Maafisa Habari wa Halmashauri

=30=

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Habari zinazoendelea hivi sasa

SERIKALI KUWEZESHA VIJANA KUKOPA

Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Iringa Serikali itaendelea kuwawezesha vijana kwa kuwatengenezea mazingira mazuri ya mikopo ili waweze k...