Jumapili, 20 Julai 2014

UJASIRI WA CHIFU MKWAWA WASAIDIA UHURU NCHI ZA KUSINI MWA AFRIKA



Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Historia ya chifu Mkwawa ya ujasili wa kupinga ukoloni imelisaidia Taifa wakati wa kupigania uhuru nchini na nchi za jirani kusini mwa Afrika.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mizengo Pinda katika hotuba yake ya kilele cha maadhimisho ya kumbukumbu ya chifu Mkwawa na utamaduni wa mkoa wa Iringa, iliyosomwa kwa niaba yake na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Dkt. Binilith Mahenge na kufanyika katika kijiji cha Kalenga nje kidogo ya mji wa Iringa.
Pinda “historia ya chifu Mkwawa ya ujasiri na kupinga ukoloni imelisaidia Taifa letu wakati wa kupigania uhuru na pia wakati wa harakati za kudai uhuru kuzisaidia nchi jirani za kusini mwa Afrika. Hivyo, inatupasa sote kuendelea kudumisha mila, desturi na tamaduni zetu kwa ustawi wa jamii na Taifa kwa ujumla”.
Waziri Mkuu amesema kuwa historia ya Mkwawa na utamaduni wa mkoa wa Iringa umechangia kwa wageni wengi kutoka nchi za nje kupenda kutembelea mkoa huo. Amesema lengo la wageni hao kutembelea ni kuona maeneo ya kihistoria na kitamaduni yanayohusiana na Mtwa Mkwawa. Amesema kuwa kutokana na nafasi hiyo ya kimkakati ndiyo iliyopelekea mkoa huo kuteuliwa kuwa kitovu cha utalii kwa nyanda za juu kusini mwaka 2009.
Pinda amewataka wananchi wa mkoa wa Iringa kuendelea kuenzi na kuthamini utamaduni wao. Amesema utamaduni huo ni kichocheo kikubwa katika kukuza maendeleo ya wananchi na Taifa.
Aidha, ametoa rai kwa wananchi wa ndani na nje kujitokeza na kuwekeza katika sekta ya utalii katika ukanda Kusini kwa lengo la kuinua sekta hiyo ili iweze kutoa mchango unaostahili katika pato la Taifa. Amesema kuwa serikali kwa kipindi hiki inaelekeza nguvu katika ukanda wa kusini.
Akiongelea maadhimisho hayo kufanyika mwaka huu, mwananchi Weslaus Chaula amesema kuwa hilo ni jambo jema kwa sababu kuenzi utamaduni hasa wa shujaa Mkwawa ni ustaarabu. Amesema kuwa watu wote waliostaarabika wana taratibu za kuenzi na kuhifadhi utamaduni wao. Amesema kuwa anatarajia maadhimisho hayo yatakuwa endelevu ili kukijengea ujasiri kizazi kijacho kwa kutumia historia ya chifu Mkwawa.
Maadhimisho ya kumbukumbu ya chifu Mkwawa yaliongozwa na kaulimbiu isemayo “utamaduni wa mkoa wa Iringa ni chachu ya maendeleo ya utalii”. Wakati huohuo Waziri, Dkt. Mahenge alisimikwa rasmi kuwa miongoni mwa chifu wasaidizi wa wahehe.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma alisema kuwa maadhimisho hayo yanalenga kuuelimisha umma kuhusu umuhimu wa kudumisha utamaduni wa mkoa wa Iringa kwa maendeleo ya wananchi na Taifa kwa ujumla.
=30=

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Habari zinazoendelea hivi sasa

SERIKALI KUWEZESHA VIJANA KUKOPA

Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Iringa Serikali itaendelea kuwawezesha vijana kwa kuwatengenezea mazingira mazuri ya mikopo ili waweze k...