Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Wananchi wa Mkoa wa Iringa wametakiwa
kujitokeza kwa wingi katika wiki ya mwisho ya uboreshaji wa daftari la kudumu
la wapiga kura.
Kauli hiyo imetolewa na Mratibu wa
Mkoa wa zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura, Bw. Wilfred
Myuyu katika mahojiano maalumu ya hali halisi ya zoezi hilo katika mkoa wa
Iringa yakiyofanyika ofisini kwake leo.
Bw. Myuyu amesema kuwa lengo la Tume
ya Taifa ya uchaguzi ni kuhakikisha kila mtanzania mwenye sifa anaandikishwa
katika Daftari hilo la kudumu. Amesema kuwa Mkoa wa Iringa pia umedhamilia
kuandikisha wananchi wote wenye sifa katika daftari hilo. Ametoa wito kwa
wananchi wote wenye sifa kujitokeza mapema katika zoezi hilo ili waweze
kuandikishwa. Amewataka wananchi kujiandikisha mapema na kuacha tabia ya
kusubiri siku ya mwisho ambapo watu huwa wengi katika mistari ya uandikishaji.
Akiongelea hamasa ya wananchi katika
mkoa wa Iringa, Mratibu wa Mkoa amesema kuwa hamasa ni kubwa kwa wananchi wa
Mkoa wa Iringa. Amesema kuwa mkoa umepanga awamu nne za uandikishaji. Amezitaja
awamu hizo kuwa ni awamu ya kwanza iliyoanza tarehe 30/4/2015-6/05/2015, awamu
ya pili 8/5/2015-14/5/2015, awamu ya tatu 16/5/2015-22/5/2015 na awamu ya nne 24/5/2015-30/5/2015.
Amesema kuwa katika awamu tatu zilizopita hamasa ya wananchi imekuwa ni kubwa.
“Hadi kufikia tarehe 22/5/2015 jumla ya
wapiga kura 391,579 sawa na asilimia 79.3 ya lengo la uandikishaji mkoa
walikuwa wamejiandikisha”.
Bw. Myuyu amesema kuwa changamoto
kubwa ni wingi wa watu wanaopenda kujiandikisha siku ya mwisho na vituo
kulazimika kuongeza muda wa uandikishaji. Amesema kuwa awamu ya mwisho itatoa
matokeo mazuri.
Bw. Myuyu ametoa wito kwa wananchi
kuendelea kudumisha amani na utulivu katika zoezi hilo ili liwe la mafanikio na
kuwataka kuwaibua wale wote wasio na sifa za kujiandikisha katika daftari la
kudumu la wapiga kura.
Awali Bibi. Rehema Mohamed Sadiki,
mkazi wa mtaa wa Maliwa amepongeza zoezi la uandikishaji katika mtaa wake na
kusema kuwa waandikishaji wapo makini na wana kasi ya kulidhisha. Aidha, ametoa
rai kwa wananchi wote kujitokeza mapema kuboresha taarifa zao kabla ya siku ya
mwisho ili kuweza kutumia fursa na haki yao kikatiba ya kuchagua viongozi
wanaofaa.
Zoezi la uboreshaji wa daftari la
kudumu la wapiga kura limeanza tarehe 30/4/2015 Mkoani Iringa na linatarajiwa
kumalizika tarehe 30/5/2015 wakati mkoa ukitarajia kuandikisha wapiga kura
493,277.
=30=
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni