Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Vyama vya siasa mkoani Iringa
vimetakiwa kudumisha amani na utulivu katika kipindi hiki kuelekea uchaguzi
mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa
wa Iringa, Amina Masenza alipokuwa akifunga kikao maalum cha Kamati ya Ushauri
ya Mkoa wa Iringa kilichofanyika katika ukumbi wa Siasa ni Kilimo.
Masenza amesema “Iringa hatuhitaji vurugu kwa wananchi wetu. Vyama vya siasa waambieni
wafuasi wenu kuwa Iringa hatuhitaji vurugu kwa namna yoyote katika kipindi chote
kuelekea uchaguzi mkuu na katika uchaguzi mkuu wenyewe. Kamati ya Ulinzi na Usalama
ipo makini muda wote na itashughulika na wote watakaojipanga kufanya vurugu”.
Amewataka kuingia katika uchaguzi mkuu wakiwa wamoja na kudumisha mshikamano
uliopo.
Mkuu wa Mkoa amewataka kuendelea
kushirikiana na kutengeneza timu itakayowezesha kufanikisha majukumu ya
kiutekelezaji. Amepongeza juhudi na usimamizi wa Katibu Tawala Mkoa wa Iringa,
Wamoja Ayubu katika mchakato wa kuanzisha na kusimamia ugawanaji wa watumishi
na mali baina ya Halmashauri ya wilaya ya Mufindi na Halmashauri ya Mji wa Mafinga.
“Napongeza kazi nzuri iliyofanywa na
Katibu Tawala Mkoa kutokana na uzoefu wake. Yapo maeneo ambayo mgawanyo
ulifanyika vibaya kwa kupeleka watu wasiokubalika eneo moja na kufanya utendaji
wa kazi kuwa mgumu” alisema Masenza.
Awali akijibu hoja juu ya
ushirikishwaji wananchi kwa lengo la kuondoa migongano baina ya wananchi na serikali
katika uanzishwaji wa Halmashauri ya wilaya ya Kilolo iliyotolewa na Mwenyekiti
wa Halmashauri ya wilaya ya Iringa, Stephen Mhapa, Katibu Tawala Mkoa wa Iringa,
Wamoja Ayubu amesema kuwa mgawanyo uliofanyika ni shirikishi na umezingatia
hali na mahitaji ya kijiografia hasa maeneo ambayo wananchi walikuwa wanapata
changamoto zaidi. Amesema kuwa ramani inaendelea kuandaliwa inayoonesha
uhalisia wa maeneo yaliyogawanywa. Akijibu hoja ya changamoto ya mawasiliano,
amesema kuwa lengo la mgawanyo huo ni kufanya huduma ya mawasiliano iwe bora
kwa wananchi wote.
=30=
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni