Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Iringa
imeridhia kwa kauli moja mapendekezo ya kugawa Jimbo la uchaguzi la Kilolo
lililopo katika wilaya ya Kilolo kwa lengo la kuboresha utoaji wa huduma bora
kwa wananchi.
Katika kikao maalum cha Kamati ya Ushauri
ya Mkoa wa Iringa kilichofanyika katika ukumbi wa Siasa ni Kilimo mjini Iringa
kimepitisha kwa kauli moja mapendekelezo ya kugawa Jimbo la uchaguzi la Kilolo
na kuanzishwa kwa Jimbo jipya la Ilula.
Akiwasilisha mapendekezo ya kugawa Jimbo
la uchaguzi la Kilolo, Kaimu Katibu Tawala Msaidizi, Sehemu ya Mipango na
Uratibu katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Conrad Millinga amesema “wilaya ya Kilolo ipo katika mchakato wa
kuanzisha Halmashauri mpya ya wilaya ya Ilula, kwa sababu hiyo tunawasilisha
mapendekezo ya kuligawa Jimbo la uchaguzi la Kilolo kuwa Majimbo mawili ya
uchaguzi yaani Jimbo la uchaguzi la Kilolo na Jimbo la uchaguzi la Ilula”.
Amesema kuwa mapendekezo haya yamepitishwa na vikao vya kisheria katika ngazi
ya Halmashauri na wilaya na kuvitaja vikao vya Kamati ya Fedha, Mipango na
Utawala, Baraza la Madiwani na Kamati ya Ushauri ya Wilaya. Amesema kuwa vikao
vyote vimeridhia uanzishwaji wa Jimbo la uchaguzi la Ilula ili kuwezesha kila
Halmashauri kuwa na Jimbo lake la uchaguzi na kuepuka Jimbo moja kuwa ndani ya
Halmashauri mbili. Sababu nyingine ameitaja kuwa ni kusaidia upatikanaji wa
rasilimali na kurahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Akiongelea hali ya Majimbo
yanayopendekezwa kugawanywa, Millinga amesema kwa mujibu wa Ofisi ya Taifa ya
Takwimu makadirio ya idadi ya watu katika wilaya ya Kilolo ifikapo Oktoba, 2015
ni watu 235,556. Amesema Majimbo yanayopendekezwa yanakadiriwa kuwa na idadi ya
watu kama ifuatavyo; Jimbo la Kilolo watu 115,164 na Ilula watu 120,392. Aidha,
ukubwa wa Jimbo la kilolo ni Km za mraba 2,642.5 na Jimbo la Ilula ni Km za
mraba 5,232.1.
Mipaka ya kiutawala, Millinga amesema
kuwa Jimbo la Kilolo litakuwa na Kata 12 wakati Ilula Kata 14.
Afisa Habari ya Wilaya ya Kilolo,
Filemon Namwinga amesema kuwa mapendekezo ya kugawa Halmashauri ya wilaya ya
Kilolo na Jimbo la uchaguzi la Kilolo yanafanyika katika muda muafaka.
Amepongeza vyombo vya maamuzi kufikia hatua hiyo na kusema huo ni uamuzi wa
kimkakati unaolenga kuwafikishia wananchi huduma bora. Amesema kuwa sababu za
kijiografia na ukubwa wa maeneo ni changamoto kuwa katika kufikisha huduma
stahiki kwa wananchi. “Kwa mfano changamoto ya kijiografia kama ukanda wa juu
wenye msimu mrefu wa masika na msimu mfupi sana wa kiangazi tofauti na ukanda
wa chini wenye msimu mrefu wa kiangazi na masika muda mfupi sana.
=30=
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni