Ndugu
wananchi wa Mkoa wa Iringa, awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa
Rehema kwa kuujalia Mkoa wetu amani na utulivu katika kipindi cha mwaka mzima
wa 2015. Aidha, ninawapongeza sana wananchi kwa kudumisha amani na utulivu kwa
kipindi chote cha mwaka 2015.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Amina Masenza |
Ndugu
wananchi,
Mwaka
huu kulikuwa na uchaguzi Mkuu ambao umepelekea kupata uongozi mpya wa nchi yetu
katika ngazi ya Urais, Ubunge na Udiwani. Ninapenda kutoa pongezi zangu za
dhati kwa Mheshimiwa. Dkt. John Pombe
Magufuli kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa awamu ya tano ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Wabunge na madiwani wote waliyochaguliwa kuwa wawakirisha wa
wananchi. Ninawatakia utumishi mwema.
Aidha,
napenda kuvipongeza vyama vyote vya siasa vilivyoshiriki katika Uchaguzi Mkuu,
ambapo wakati wote licha ya tofauti za itikadi vilihakikisha vinadumisha amani,
utulivu na umoja wa kitaifa. Hali hiyo imeuthibitishia ulimwengu kwamba
Tanzania inaukomavu mkubwa wa kisiasa. Ninawapongezeni sana wananchi wa Iringa
kwa kupita katika kipindi hicho kigumu tukiwa na amani na umoja.
Ndugu
wananchi,
Pamoja
na mafanikio mengi tuliyoyapata katika mwaka 2015 yalitokea baadhi ya matukio
yaliyoutia simanzi Mkoa wetu. Miongoni mwa matukio hayo ni kutokea kwa ajali
mbaya za mabasi ya abiria katika Wilaya za Kilolo na Mufindi ambazo
zilisababisha vifo vya Watanzania wenzetu. Tukio jingine la kusikitisha ni
ajali za moto katika Shule ya Sekondari ya Idodi na William Lukuvi Wilaya ya
Iringa vijijini ambazo zilisababisha mshituko mkubwa kwa wanafunzi na kuathiri
utaratibu wa masomo pamoja na kusababisha hasara kubwa ya vifaa na majengo.
Aidha,
changamoto nyingine ni hali ya ukame ambayo imesababisha upungufu wa chakula
kwa baadhi ya maeneo ya Mkoa wetu, hususani Wilaya ya Iringa vijijini na
Kilolo.
Ili
kuhakikisha wananchi waliokabiriwa na njaa wanapata chakula, Serkiali kupitia
Ofisi ya Waziri Mkuu imeshatoa tani 850
za chakula ambapo tani 500 zimegawiwa kwa wananchi wenye njaa, na tani
350 tunaendelea kuzisafirisha Kutoka ghara la Hifadhi ya chakula ya Taifa
Mbakambako na kuzipeleka katika maeneo yenye uhaba wa chakula. Ninatambua bado
shida ya chakula ni kubwa ninaomba sana mtumie hicho mlicho nacho vema.
Serikali
inendeleza maombi kuona tunapata kingine na wafanya biashara wanajitokeza kutoa
huduma ya kutuuzia chakula muda wote. Kama tutapata kibali cha kununua kutoka
hifadhi ya chakula ya taifa ni vema mhakikishe chakula hicho kinafika kwa wenye
njaa na kuuzwa kwa bei iliyoelekezwa. Atakayebainika kukiuka taratibu zilizo
wekwa hatutasita kumchukulia hatua za kisheria.
Napenda
kuwahakikishia wananchi kwamba uongozi wa Mkoa wa Iringa umejipanga vizuri
katika ngazi zote za serikali kukabiliana na changamoto hizo ili wananchi na
Mkoa wetu uendelee kuwa sehemu salama kwa wananchi kuishi na kufanya shughuli
za maendeleo.
Ndugu
Wananchi,
Tunavyoelekea
kuanza mwaka mpya 2016 ni muhimu kila mmoja wetu ajiwekee malengo na vipaumbele
ambavyo atavitekeleza mwaka 2016. Mtu asiye na malengo ni sawa na mtu
anayetembea katika giza na asiyejua aendako. Kwa upande wetu kama serikali
tumejiwekea vipaumbele vinne (4)
ambavyo ni:-
i.
Kuhakikisha tunasimamia kikamilifu
utekelezaji wa mpango wa usafi wa mazingira na ujenzi wa vyoo bora kwa kila
kaya hadi ifikapo mwezi Februari 2016.Tutasimamia kikamilifu sheria za usafi wa
mazingira ili sasa wanachi wote tujenge mazoea ya kuishi katika mazingira
yaliyosafi na salama.
ii.
Kusimamia na kutekeleza kikamilifu mpango
wa kuhakikisha kila mwananchi anafahamu umuhimu wa kupata lishe bora. Hii ni
pamoja na kutilia mkazo wa lishe bora kwa akina mama wajawazito na watoto
wadogo ili kujenga ubongo wa watoto katika siku za mwanzo za maisha yao (siku
1000 tangia uhai wa mtoto). Lengo ni kuhakikisha wananchi wote wanakuwa na afya
njema na kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo.
iii.
Lengo la tatu ni kuendelea kutekeleza
mikakati ya kupunguza kiwango cha maambukizi ya UKIMWI. Kama mjuavyo Mkoa wetu
ni wa pili kitaifa kwa kuwa na kiwango cha juu cha maambukizi ya VVU/UKIMWI
ukiwa na asilimia 9.1.Hii ni changamoto kubwa tunapaswa sote tuikabiri. Ni
lazima kila mmoja ahakikishe anajilinda mwenyewe na kumlinda mwenzake. Kila
mmoja wetu aamini kwamba Iringa bila UKIMWI inawezekana.
iv.
Kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanajiunga
na mfuko wa Afya ya Jamii (CHF). Tuna amini mfuko huu ni ukombozi kwa wananchi
kwa upande wa huduma za afya .Mfuko huu utawasaidia wananchi kuepuka gharama
kubwa za matibabu. Katika Mfuko huu mwananchi anachangia Tsh. 10,000/= na
serikali inamwongezea Sh. 10,000/= matibabu mwaka mzima. Natoa wito kwa
wananchi wote kuchangamkia fursa hii. Kila hospitali, Kituo cha afya na
zahanati, zihakikishe wananchi wanaotaka kujiunga na mfuko huu wanasajiliwa.
Naviomba vyombo vya habari kusaidia kutoa elimu kwa wananchi juu ya jambo hili,
ikibidi anzisheni vipindi maalumu vya kutoa elimu ambapo wataalamu watatoa
elimu.
Ndugu
Wananchi,
Kipindi
hiki cha Mwezi Disemba na Januari ni muhimu sana katika mipango ya maendeleo ya
Mkoa wetu. Tuwaandikishe wanafunzi wa darasa la kwanza na kuwapeleka shule
wanafunzi wanaoanza kidato cha kwanza.
Kila
Mkulima ahakikishe anazingatia kanuni za kilimo bora ili kupata tija ya
kutosha. Na hapa ni lazima kulima kwa kutumia ushauri wa wataalamu wa kilimo na
kuachana na kilimo cha mazoea. Kwa wananchi wanaoishi katika maeneo yanayopata
mvua kidogo ni lazima wapande mazao ambayo yanahimili ukame hususani zao la
mtama. Muhimu kuchukua tahadhari kwa wote wanaolima mabondeni kuepuka
mmomonyoko wa ardhi usiathiri nguvu kazi iliyotumika kwa kuzoa mazao
mtakayopanda.
Mamlaka ya hali ya hewa imetahadharisha kwamba mwaka huu kutakuwa
na mvua nyingi hivyo tuchukue tahadhari mapema.
Ndugu
Wananchi,
Mwisho,
Leo tunasherehekea Maulidi ya kuzaliwa Mtume Muhamad (SWA) rehema na amani ziwe
juu yake, kesho siku kuu ya Krismas na siku chache zijazo tutasherehekea
kuukaribisha mwaka mpya 2016. Ninaomba tusherehekee kwa amani na utulivu huku
tukijua kwamba kuna maisha baada ya sherehe hizi. Ninapenda kuwahakikishieni
kwamba serikali itahakikisha wakati wote wa sherehe kunakuwa na amani na
utulivu. Vyombo vyetu vya dola vipo macho na thabiti kabisa kutekeleza jukumu
hilo. Kwa wale wachache ambao wanatabia ya kutumia siku za sherehe kufanya
vitendo vya uhalifu na uvunjifu wa amani, watachukuliwa hatua kali za kisheria.
Kila
familia iwe na tahadhari za kiulinzi ili kutotoa mwanya kwa uhalifu wowote.
Wazazi waangalieni watoto na kwa pamoja tuwalinde, hakuna Disco Toto na watoto wakitembea wawe na waangalizi. Tafadhali
mpende mwanao.
Ninawatakia
Siku kuu njema ya Maulidi, Krismas na Mwaka mpya 2016.
Ahsanteni
kwa kunisikiliza.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni