Na. Ofisi ya mkuu wa Mkoa
Mashirika
yasiyo ya kiserikali yanayopambana na maambukizi ya virusi vya Ukimwi
yametakiwa kujitathmini na kuunganisha nguvu katika kupunguza maambukizi mapya
ya virusi vya Ukimwi mkoani Iringa.
Kauli
hiyo ilitolewa na mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza alipokuwa akifungua
kikao cha kupitia utekelezaji wa mpango mkakati wa Mkoa wa kudhibiti maambukizi
ya mapya ya virusi vya Ukimwi mkoani Iringa kikao kilifanyika katika ukumbi wa
chuo kikuu Huria mjini Iringa.
Masenza
alisema kuwa mashirika yasiyo ya kiserikali yote yanayoratibu masuala ya Ukimwi
lazima yaache alama njema katika mkoa wa Iringa. Aliwataka kujitathmini na kuja
na mkakati utakaosaidia kupunguza maambukizi mapya ya virusi vya Ukimwi.
Alisema
kuwa matokeo ya utafiti wa VVU na Ukimwi umebainisha kuwa kiwango cha
maambukizi kimeongezeka kwa asilimia 2.2 mkoani Iringa. Alisema kuwa ongezeko
hilo ni kubwa sana.
“Lazima tupitie na
kufanya tathmini ya mikakati yetu na mwanzo wa mwaka kuanza upya kwa kudumisha
ushirikiano baina yetu. Yawezekana ushirikiano na dhamira ya kweli miongoni mwetu
katika kupunguza maambukizi mapya haijaimarika” alisema Masenza.
Aliwataka
wadau hao kuona kuwa wana deni kwa wananchi wa mkoa wa Iringa. “Kila mmoja ajisikie vibaya baada ya lile
lengo tulilolitarajia hatukulifikia. Nyie wataalam lazima muweze kushauri
vizuri ili tuweze kufikia dhamira ya kupunguza maambukizi mapya” alisema Masenza.
Awali
afisa maendeleo ya jamii Mkoa wa Iringa, Menrad Dimoso alisema kuwa hicho ni
kikao cha kazi kinacholenga kupitia utekelezaji wa mpango mkakati wa Mkoa wa
kupambana maambukizi mapya ya virusi vya Ukimwi. Alisema kuwa kikao hicho
kimeshirikisha wadau mbalimbali wa mapambano dhidi ya virusi vya ukimwi na
halmashauri za Mkoa wa Iringa.
Matokeo ya utafiti
wa VVU na UKIMWI (2016/17) yaliyotoka hivi karibuni yalibainisha kuwa
maambukizi ya VVU Mkoani Iringa yameongezeka kutoka asilimia 9.1 (2011/12)
kufikia asilimia 11.3 (2016/17).
=30=
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni