Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Wanafunzi
wanufaika wa mpango wa kunusuku kaya masikini nchini (TASAF) kupitia ruzuku ya
elimu wametakiwa kuwashirikisha walimu katika masuala yanayohusu taaluma na
ustawi wao ili waweze kufaulu.
Kauli
hiyo ilitolewa na Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Wamoja Ayubu alipokuwa akiongea
na wanafunzi wanufaika wa TASAF wa shule ya msingi Kitwiru iliyopo Kata ya
Kitwiru Manispaa ya Iringa hivi karibuni.
Ayubu
alisema “watoto wangu mpo hapa kwa ajili ya kusoma na wote kufaulu, si ndiyo.
Walimu wenu wapo hapa kwa ajili ya kuwafundisha na kuwasaidia kufaulu hivyo
msiwaogope. Wafuateni kwa ushauri na maelekezo ili muweze kusoma vizuri na wote
kufaulu, sawa”.
Alisema kuwa serikali inatoa fedha kwa wanafunzi hao kiasi cha
shilingi 2,000 kwa mwezi ili waweze kununua mahitaji ya muhimu ya shule.
Serikali inataka kuona kila mtoto wa kitanzania anasoma vizuri ili aweze
kujitegemea na kuchangia katika kukuza pato la Taifa.
Nae
mratibu wa TASAF Mkoa wa Iringa, William kingazi aliwataka wanafunzi hao kusoma
kwa bidii na kuwa wasikivu kwa walimu na wazazi. “Nyie wanafunzi lazima muwe na
ndoto kwamba mtakapomaliza masomo mnataka kuwa watu wa aina gani. Ndoto hizo
ziwasaidie kusoma kwa bidii ili muweze kuzifikia” alisema Kingazi.
Aidha,
aliwataka walimu kuwafuatilia wazazi wanufaika wa mpango wa TASAF ili waweze
kuwanunulia watoto sare za shule kwa wale ambazo sare zao zimechanika ili
wasijione tofauti na wengine.
Katibu
Tawala Mkoa wa Iringa alifanya ziara maalum ya ufuatiliaji kwa wanafunzi
wanufaika wa mpango wa TASAF kupitia elimu katika Manispaa ya Iringa kujifunza
changamoto zinazowakabili. Katika ziara hiyo aliambatana na mratibu wa TASAF
Mkoa, afisa mipango, mhasibu, mkaguzi wa ndani na afisa habari.
=30=
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni