Na. Mwandishi Maalum Iringa
Makatibu
Tawala wa Wilaya za Mkoa wa Iringa wametakiwa kufanya vikao vya kila robo mwaka
na watumishi wanaowasimamia ili kutatua kero zinazowakabili.
Agizo
hilo lilitolewa na Katibu Tawala msaidizi, Sehemu ya Menejimenti ya rasilimali
watu katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Lucas Kambelenje alipokuwa
akiongea na watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Iringa katika ukumbi wa
mikutano wa ofisi hiyo jana.
Kambelenje
alisema kuwa watumishi katika ngazi ya wilaya wamekuwa na kero nyingi ambazo utatuzi
wake upo katika ngazi ya wilaya. Alisema suluhisho la kero hizo ni Makatibu Tawala
wa Wilaya kufanya vikao na watumishi wote wanaowasimamia ili kusikiliza na kuondoa
kero zinazowakabili. “Watumishi wengi
wanakabiliwa na kero ya kutokuelewa baadhi ya miundo na miongozo ya serikali.
Na jambo hili na ufafanuzi wake ni jukumu lenu Makatibu Tawala wa Wilaya.
Kufanya hivyo kutaondoa kero na manung’uniko miongoni mwa watumishi
mnaowasimamia na hali ya ofisi zenu na utendaji itakuwa bora zaidi” alisema
Kambelenje.
Akiongelea
suala la mipango na bajeti, Kambelenje aliwataka Makatibu Tawala wa Wilaya
kuwashirikisha watumishi katika mipango na bajeti ya wilaya. Alisema kuwa
ushirikishaji watumishi hao kutawajengea uelewa mpana wa hali ya bajeti katika
ofisi zao na kuondoa malalamiko. Alisema kuwa watumishi wanalalamika kutokana
na kutofahamu hali ya bajeti katika ofisi hizo.
Wakati
huohuo, Afisa Utumishi katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Olgatho Mwinuka
aliwataka watumishi hao kufuata taratibu katika kuomba likizo mbalimbali
ikiwemo likizo ya mwaka. “Likizo ya mwaka
ni haki ya kila mtumishi. Lakini likizo hiyo inataratibu zake kama zilivyoelezwa
katika Kanuni za kudumu za Utumishi wa Umma, toleo namba tatu la mwaka 2009
kifungu H”. Alisema kuwa mtumishi wa umma anatakiwa kuomba likizo yake ya
mwaka ndani ya mzunguko wa likizo hiyo kwa kuandika barua ya maombi siku 14
kabla ya kuanza likizo na kuambatanisha na fomu ya maombi ya likizo husika.
Alisema kuwa mtumishi wa umma haruhusiwi kuondoka katika kituo chake cha kazi kabla ya kujibiwa kuwa ruhusa yake
imekubaliwa kwa barua na kupatiwa nakala ya fomu ya likizo hiyo. “Mtumishi wa umma kuondoka kituoni na kuanza
likizo bila kupitishwa na mwajili wake ni utoro kazini na mtumishi huyo
anatakiwa kuadhibiwa kwa mujibu wa taratibu za utumishi wa umma. Ikumbukwe kuwa
mwajili anaweza kusitisha likizo ya mtumishi kutokana na majukumu ya kazi
yaliyopo kwa wakati huo” alisisitiza Mwinuka.
Aliongeza
kuwa likizo ya mwaka ya mtumishi ni siku 28 na mtumishi atalipwa nauli ya
likizo kila baada ya kupita likizo moja. Aliwataja wanufaika wa malipo ya nauli
ya likizo kuwa ni mtumishi mume au mke, watoto au wategemezi wanne baada ya
kuwasilisha vyeti vya kuzaliwa au hati ya kiapo toka mahakamani kwa wategemezi.
Ofisi
ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa inaadhimisha wiki ya Utumishi wa Umma tarehe
16-23/6/2017 kwa kutembelea watumishi wa makao makuu ya mkoa, Ofisi za Wakuu wa
Wilaya na hospitali ya rufaa ya Mkoa na kutoa mada mbalimbali zinazohusu haki
na wajibu wa mtumishi wa umma, mapambano dhidi ya maambukizi ya virusi vya
ukimwi, mapambano dhidi ya rushwa na kusikiliza na kutatua kero za watumishi.
=30=
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni