Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Mkuu wa Mkoa wa Iringa
amesema kuwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar umeleta mafanikio makubwa
katika nyanja zote nchini.
Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Iringa ambaye ni Kaimu Katibu Tawala Mkoa, Bibi. Scolastica Mlawi (katikati) akifuatilia burudani mbalimbali |
Kauli hiyo imetolewa na
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma katika hotuba yake iliyosomwa kwa
niaba yake na Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Iringa Scolastica Mlawi katika Maadhimisho
ya miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar yaliyofanyika katika kijiji
cha Kasanga, Kata ya Kasanga, Tarafa ya kasanga wilayani Mufindi.
Dkt. Ishengoma amesema “muungano
umeleta manufaa makubwa katika nyanja za kisiasa, kiuchumi, kijamii na
kiutamaduni, jukumu letu ni kuuenzi, kuudumisha na kuuimarisha kwa masilahi ya
vizazi vya sasa na vijavyo”. Amesema
kuwa manufaa yatokanayo na Muungano huu ni pamoja na kudumishwa kwa amani,
upendo, umoja, mshikamano na ushirikiano miongoni mwa jamii ya Tanzania Bara na
Tanzania visiwani.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa
amesema kuwa waasisi wa Muungano walikubaliana kushirikiana katika mambo mengi.
Ameyataja baadhi ya mambo hayo kuwa ni katiba na serikali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, mambo ya nchi za nje, ulinzi na usalama, polisi, mamlaka
juu ya mambo yanayohusika na hatari. Mambo mengine ni pamoja na uraia,
uhamiaji, mikopo na biashara za nje, utumishi katika serikali ya Jamhuri ya
Muungano na kodi inayolipwa na watu binafsi na mashirika. Ameyataja mambo
mengine kuwa ni ushuri wa forodha na ushuru wa bidhaa zinazotengenezwa nchini
unaosimamiwa na idara ya forodha pamoja na ushirikiano wa bandari, usafiri wa
anga na posta na simu.
Dkt. Ishengoma amewataka
wananchi wote mkoani Iringa kuhakikisha wanaendeleza yale yote mambo mazuri
yaliyoachwa na waasisi wa Muungano na kuyaboresha pale inapobidi. Aidha,
amewataka wananchi wote kujitokeza na kushiriki katika shughuli za maendeleo
ili kujiletea maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Maadhimisho ya miaka 50 ya
Muungano wa Tanzania yameongozwa na kauli mbiu isemayo “Utanzania Wetu ni
Muungano Wetu, Tuulinde, Tuuimarishe na Kuudumisha”.
=30=
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni