Na. Dajari Mgidange
Wazazi wametakiwa
kuwapeleka watoto wao wenye umri chini ya miaka miwili kwenye vituo vya huduma
za afya kupatiwa chanjo dhidi ya magonjwa mbalimbali.
Kaul;I hiyo imetolewa na
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma alipokuwa akizindua wiki ya
chanjo katika mkoa wa Iringa uzinduzi uliofanyika katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa.
Dkt. Christine amesema
kuwa kumekuwa na ongezeko la watoto ambao hawajapata na wengine kutokamilisha
chanjo zao matokeo yake kusababisha milipuko ya magonjwa ya mara kwa mara hasa
ugonjwa wa surua. Amesema katika jitihada za kuzuia milipuko hiyo Tanzania
inatarajia kutoa chanjo ya pili ya surua mwaka huu. Ametoa wito “kwa wazazi na
walezi kuwapeleka watoto wote wenye umri chini ya miaka miwili ambao hawajapata
chanjo au hawajakamilisha chanjo zao kwenye vituo vya huduma za afya wakiwa na
kadi zao za kliniki lakini pia watoto ambao hawana kadi wapelekwe watapewa kadi
na chanjo” alisisitiza Dkt. Ishengoma.
Amesema “kila mmoja wetu
anawajibu wa kuhakikisha kuwa mtoto wake, mtoto wa jirani au mlengwa mwingine
yeyote anapewa chanjo ili kuzuia asipatwe na maradhi ambayo yanakingwa na
chanjo na asiwe hatari kwa wengine kwa kuwaletea ugonjwa”. Amesema kuwa chanjo
ni jukumu la jamii nzima na hutolewa bila malipo yoyote na kuwahakikishia kuwa
hazina madhara yoyote.
Mkuu wa Mkoa amesema kuwa
wiki ya chanjo ni fursa ya kutoa ujumbe kuhusu chanjo mpya za kuzuia ugonjwa wa
Nimonia na Kuhara kwa watoto na kuhamasisha jamii kufika vituoni ili kupata
maelezo zaidi na huduma hiyo. Ujumbe wa wiki ya chanjo ni “Jamii iliyokamilisha
chanjo ni jamii yenye Afya” ukiongozwa na kaulimbiu isemayo “Chanjo ni
jukumu letu sote”.
Amesema kuwa chanjo ni
mkakati muafaka katika kutokomeza maradhi na kupunguza vifo vya watoto, hivyo
kupunguza gharama kubwa kwa famila na Taifa kwa ujumla. Ameongeza kuwa chanjo
huchangia kupunguza vifo vya watoto kati ya milioni mbili (2) hadi milioni tatu
(3) Duniani kila mwaka yakiwemo maradhi ya Nimonia na Kuhara ambayo yamekua ni
chanzo cha vifo vingi. Ameyataja magonjwa yanayokingwa hapa nchini na chanjo
kuwa ni kifua kikuu, dondakoo, polio, surua, pepopunda, homa ya ini, homa ya
uti wa mgongo, kichomi na kuhara.
Tanzania inaungana na nchi
nyingine katika kuadhimisha wiki ya chanjo Duniani tarehe 24-30 April 2014. Katika
mkoa wa Iringa ilizinduliwa katika kijiji cha Ulata Kata ya Wasa, Tarafa ya Kiponzelo
katika Halmashauri ya Wilaya ya Iringa.
=30=
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni