Jumatatu, 5 Mei 2014

HOSPITALI YA WILAYA MUFINDI UADILIFU KWANZA



Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Wafanyakazi wa hospitali ya wilaya ya Mufindi wametakiwa kufanya kazi kwa uadilifu na upendo ili kuweza kutoa huduma bora kwa wananchi.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mahamod Mgimwa alipokuwa akiongea na wafanyakazi na wadau mbalimbali wa sekta ya afya wilayani Mufindi muda mfupi baada ya uzinduzi wa jengo la akina mama wajawazito katika hospitali ya wilaya ya Mufindi.

Mgimwa amesema “Ombi langu kwenu pamoja na misaada hii lazima tuitumie kwa uadilifu mkubwa katika kuwahudumia wananchi”. Amesema kuwa katika kutoa huduma bora kwa wananchi suala la upendo na kujali wagonjwa lazima lipewe kipaumbele. Amewataka kumtanguliza Mungu muda wote wanapotoa huduma kwa wananchi.

Akiongelea jitihada za kuipandisha hadhi hospitali ya wilaya ya Mufindi kuwa hospitali ya rufaa, Naibu waziri huyo amesema kuwa mazungunzo yameanza na yanaendelea vizuri. Aidha, amesema kuwa muda mfupi ujao hospitali hiyo itapata madaktari bingwa.

Mgimwa ameuagiza uongozi wa wilaya ya Mufindi kuwapangia madaktari katika vituo vya afya vilivyopo vijijini. Amesema kuwa kufanya hivyo kutatoa huduma hiyo kwa wananchi wengi zaidi kuliko madaktari wengi kubaki njini na kuwanyika fursa ya kupata huduma tiba wananchi waishio vijijini. 

Katika risala ya uzinduzi wa jengo la akina mama iliyosomwa na mganga mfawidhi, Dakta Eugen Lutambi amesema kuwa hospitali ya wilaya ya Mufindi inahudumia wagonjwa wan je wapatao 120 -200 kwa siku. Amesema kuwa kwa siku hospitali hiyo inalaza wagonjwa 80 hadi 120 kwa siku. Akiongelea wanawake wajawazito waliojifungua katika hospitali hiyo kwa mwaka 2013/2014, Mganga mfawidhi amesema kuwa walikuwa 3,891 wakati akina mama 619 walijifungua kwa njia ya upasuaji.
Hospitali ya Wilaya ya Mufindi
 Akiongelea huduma zitolewazo katika jengo la akina mama, Dakta Lutambi amezitaja huduma hizo kuwa ni chumba cha upasuaji, chumba cha akina mama wanaosubiri kujifungua, chumba cha akina mama waliokwishajifungua, chumba kwa ajili ya watoto walizaliwa kabla ya muda, vyumba kwa ajili ya ofisi za madaktari na wauguzi, chumba cha kujifungulia na chumba cha kufulia nguo za wagonjwa.

Akiongelea mahitaji yanayohitajika katika jengo hilo, mganga mfawidhi amesema kuwa vifaa tiba ambavyo havijanunuliwa vinathamani ya Tsh. 801,924,000. Ameongeza kuwa wanahitajika wauguzi 30 katika jengo hilo jipya.
=30=

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Habari zinazoendelea hivi sasa

SERIKALI KUWEZESHA VIJANA KUKOPA

Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Iringa Serikali itaendelea kuwawezesha vijana kwa kuwatengenezea mazingira mazuri ya mikopo ili waweze k...