Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Mkuu wa Mkoa wa Iringa Dkt. Christine
Ishengoma ameutaka uongozi wa wilaya ya Iringa kuwashirikisha vijana katika
shughuli za kilimo ili waweze kujikwamua na umasikini.
Dkt. Ishengoma ameyasema hayo
alipotembelea skimu ya umwagiliaji ya Kiwere-Mgera kukagua utendaji wake wa
kazi katika ziara ya kukagua shughuli za maendeleo wilayani Iringa.
Mkuu wa Mkoa aliwashuhudia baadhi ya
vijana wakijishughulisha na kilimo katika skimu hiyo. Amesema kuwa lengo la
serikali kujenga na kuimarisha skimu hiyo ni kuwawezesha wananchi waweze
kujihusisha na kilimo kikamilifu. Amesema lengo la serikali ni kuhakikisha
wananchi wanafanya kilimo cha uhakika na chenye tija.
Ameutaka uongozi wa wilaya kuwashirikisha
vijana katika sekta ya kilimo ili sekta hiyo iendelee kutoa mchango katika
maendeleo yao na mkoa kwa ujumla. Amesema kuwa vijana na kundi muhimu sana
katika jamii na nguvu kazi katika shughuli za maendeleo ya mkoa.
Dkt. Ishengoma ameagiza kuwa wakulima
katika skimu hiyo wajikite katika kilimo cha matunda mbalimbali ili kujiongezea
kipato. Ameyataja baadhi ya matunda yanayoweza kulimwa hapo kuwa ni maembe,
mapapati, matango.
Akiongelea manufaa yanayotokana na
skimu hiyo ya umwagiliaji, Mwenyekiti wa skimu ya umwagiliaji ya kiwere-mgera
Raphael Myinga amesema ametoa shukrani kwa serikali kwa ujenzi wa skimu hiyo ya
umwagiliaji inayohudumia zaidi ya hekta 350 katika wilaya ya Iringa. Amesema
kuwa skimu hiyo imekuwa na manufaa makubwa katika eneo hilo kwa sababu
imewawezesha vijana kujishughulisha katika kilimo na kuachana na masuala
mengine hasa ya kuhatarisha amani wilayani Iringa.
Amesema kuwa kutokana na
manufaa ya skimu hiyo wananchi wamenufaika na kilimo na mauzo ya mazao
yatokaanayo na kilimo. Amesema kuwa vijana wameweza kununua vyombo vya usafiri
kama pikipiki na magari na ujenzi wa nyumba pamoja na mambo mengine.
=30=
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni