Na. Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya
Mufindi
Mkuu
wa wilaya ya Mufindi Evarista Kalalu amewapongeza wafanyakazi wilayani Mufindi
kwa kazi nzuri wanayofanya katika kukuza uchumiwa wilaya hiyo.
Kauli
hiyo imetolewa katika hotuba yake iliyosomwa kwa niaba yake na Katibu Tawala
Wilaya ya Mufindi Allan Benard katika maadhimisho ya siku ya wafanyakazi
duniani iliyofanyika mjini Mafinga.
Kalalu
amesema kuwa anawapongeza wafanyakazi wote kwa kazi nzuri wanayofanya na kuinua
uchumi wa wilaya ya Mufindi. Akiongelea wafanyakazi bora amesema “nawapongeza
wafanyakazi wote watakaopewa tuzo ya kuwa wafanyakazi bora katika sehemu zao za
kazi. Hongereni sana kwa mafanikio haya. Nina uhakika kwamba wapo wafanyakazi
wengine wengi ambao wanafanya kazi kwa bidii katika maeneo yao ya kazi lakini
hawakubahatika kupata tuzo. Naomba wasikate tamaa, waendelee kuchapa
kazi. Huenda na wao watabahatika Mei Mosi ijayo”.
Aidha, amewataka wafanyakazi kufanya kazi kwa bidii,
umahiri na weledi ili kuongeza tija kwenye maeneo yao. Amesema “mnayo
nafasi kubwa ya kuchangia maendeleo ya nchi yetu na watu wake. Nawaomba muitumie vizuri nafasi
hiyo” alisisitiza Kalalu.
Akiongelea ujumbe wa kaulimbiu, Mkuu wa Wilaya ya
Mufindi amesema kuwa kauli mbiu isemayo “utawala bora utumike kutatua kero za wafanyakazi” ni
kauli mbiu yenye ujumbe mzuri ambao unasisitiza masuala yote ya maamuzi ya
kiutendaji na kiutekelezaji katika shughuli za kila siku za Serikali yazingatie
sheria, kanuni na taratibu za kiserikali zilizowekwa.
Amesema kuwa mwajiri
anapaswa kutoa ushirikiano mkubwa kwa watumishi wake ikiwa ni pamoja na wajibu
wa kutoa vitendea kazi bora, kujali usalama na masilahi ya wafanyakazi yakiwemo
masuala ya afya, mishahara inayoendana na hali halisi ya maisha kwa wakati
husika. Amesema kuwa mfanyakazi anapaswa kuelewa umuhimu wa nafasi yake katika
jamii kwa kufanya kazi kwa juhudi, maarifa na nidhamu ili kuleta tija.
Akijibu
risala ya wafanyakazi, Mkuu wa Wilaya ya Mufindi amesema kuwa Serikali imepokea
mapendekezo ya kuangalia upya suala la kodi inayotozwa kwenye mishahara ya
wafanyakazi na kupanda kwa kima cha chini cha mshahara kufikia Tshs. 315,000/=
kwa mwezi. Masuala mengine ambayo serikali inaendelea kuyafanyia kazi ni uwiano
kwa maslahi ya mifuko ya jamii na wastaafu kupewa mafao yao kwa muda muafaka. “Napenda
kuwahakikishia kuwa Serikali imepokea ushauri na mapendekezo hayo na itayafanyia
kazi na tutapeana taarifa ya maendeleo ya utekelezaje wake alisisitiza Mkuu wa
Wilaya.
Kalalu
amesema kuwa Serikali inaendelea na mikakati ya kuimarisha
utendaji kazi na uwajibikaji Serikalini ili wananchi wahudumiwe vizuri kama inavyostahili. Amesema kuwa serikali
imeanzisha mfumo mpya wa ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa maeneo ya
kipaumbele ya Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano kwa lengo ni kuboresha na
kuharakisha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025. Mfumo huo
unatokana na mifano mizuri inayotumika katika nchi kadhaa duniani ambako
umewaletea ufanisi mkubwa.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni