NA FRANK KIBIKI,
IRINGA
MKUU wa mkoa wa Iringa, Dk
Christine Ishengoma amewataka wafanyakazi wasiotimiza wajibu wao kuacha tabia
hiyo, ili kutokwamisha jitihada za
wananchi kujipatia maendeleo.
Akizungumza Katika hotuba yake,
iliyosomwa na Mkuu wa Wilaya ya Iringa Dk Letisia Warioba, katika maadhimisho
ya Mei mosi yambayo kwa mkoa huo, yalifanyika katika kijiji cha Isimani, Dk
Ishengoma alisema inasikitisha kuona kuwa wapo baadhi ya wafanyakazi ambao
badala ya kufanya kazi kwa bidii, wamekuwa wakisababisha huduma za jamii
kuzorota.
Alisema wapo baadhi ya
wafanyakazi ambao kwa maksudi wamekuwa wakiendekeza vitendo vya rushwa na
kuwafanya wananchi kukosa huduma wanazostahili kwa mujibu wa taratibu.
“Rushwa imekuwa ikisababisha
mwenye haki kudhulumiwa haki yake na kupatiwa mtu asiyestahili kupata haki hiyo,
ndugu zangu wafanyakazi siku hii tusiitumie kudai haki zetu za kulipwa vizuri
na kuandaliwa masingira mazuri ya kazi tu, bali tujiulize je tumetimiza wajibu
wetu?” alisema Dk Ishengima.
Alisema mbali na rushwa baadhi ya
wafanyakazi wamekuwa wakichelewa kufika katika maeneo yao ya kufanyia kazi jambo ambalo,
linaendelea kudumaza utoaji wa huduma.
Mbali na uchelewaji, Dk Ishengoma
alisema kuwa wapo ambao wamekuwa wakiwahi kufika kazini, lakini hawawajibiki ipasavyo
na kusababisha huduma kudorora.
Aliitaja kasoro nyingine kuwa ni
ubadhilifu wa mali
za ofisi jambo linalosababisha walengwa waliokusudiwa kukosa huduma iliyokuwa
imepangwa kutolewa kwao.
Alipiga marufuku, mavazi yasiyo
na staha kwa Wafanyakazi jambo linalosababisha kudharauliwa kwa Mfanyakazi
sambamba na kukemea tabia ya kuvujisha siri za ofisi kwa madai kuwa hilo pia ni tatizo
linalohitaji kuangaliwa kwa jicho la pekee.
Aliwapongeza wafanyakazi ambao,
kwa kipindi cha mwaka mzima wamekuwa wakitimiza wajibu wao na kuwataka wale
ambao kwa njia moja au nyingine wamekuwa wakizorotesha maendeleo, kuacha.
Alisema hatua kali z akisheria
zitaendelea kuchukuliwa kwa wafanyakazi wasiotimiza wajibu wao, ili kwa pampoja
wasaidiane kuongeza kasi ya ukuaji wa maendeleo na huduma za jamii mkoani humo.
Alivitaka vyama vya wafanyakazi,
kusaidia katika kutoa elimu kwa wanachama wao ili kila mmoja atimize wajibu
wake akiwa kazini.
“Tutimize kwanza wajibu wetu
ndipo tudai maslahi yetu, kama kila mmoja
atafanya kazi kwa bidii ni rahisi kufikia malengo ya kudai mashali yetu, uvivu,
tamaa na wizi ni adui wa maendeleo yetu,” alisema Dk Ishengoma.
Alisema serikali itaendelea
kutekeleza ahadi zake, za kutatua kero zinazowakabili wafanyakazi wa sekta zote
ili kila mmoja apate stahili yake.
Awali katika risala yao, wafanyakazi hao waliiomba serikali kuendelea kutatua
kero zinazowakabili na kukwamisha jitihada yao katika kufanya kazi.
Walizitaja kero hizo kuwa ni
pamoja na mishahara midogo, mazingira magumu ya kazi kwa baadhi ya sekta,
makato makubwa ya kodi, malipo ya madeni yao
ikiwemo hamisho na malimbikizo ya mishahara.
Mwisho
@MUITIKIO
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni