Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Wazazi mkoani Iringa
wameaswa tabia ya kuwaficha watoto wao wanapofikia umri wa kuanza shule na
kuwaandaa kwa lengo la kufanya kazi za majumbani na kuolewa.
Kauli hiyo imetolewa na
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma katika hotuba yake iliyosomwa
kwa niaba yake na mkuu wa wilaya ya Iringa, Dkt. Leticia Warioba katika
maadhimisho ya siku ya mtoto wa afrika yaliyofanyika ngazi ya mkoa katika
kijiji cha Tanangozi wilayani Iringa.
Dkt. Ishengoma amesema
kuwa ipo tabia ya baadhi ya wazazi kuwaficha watoto wao wanapofikia umri wa
kwenda shule na kuwaandaa kwa lengo la kufanya kazi za majumbani ama kuolewa.
Amesema kuwa wazazi na walezi huwasafirisha watoto wao kwenda katika miji
mikubwa kwa lengo la kufanya kazi za majumbani. Amewataka wazazi kuacha tabia
hiyo inayopelekea watoto kuishi katika mazingira hatarishi. Amezitaka familia
zote kuhakikisha watoto wanapata elimu iliyo bora na isiyo na vikwazo.
Akiongelea kaulimbiu, mkuu wa Mkoa amesema kuwa mwaka 2014 kaulimbiu ya maadhimisho
ni “kupata elimu bora na isiyo na vikwazo ni haki ya kila mtoto”. Ameitaja
kauli mbiu hiyo kuwa inayohimiza jamii mzima kufuata maelekezo ya sheria namba
2 ya mtoto ya mwaka 2009 pamoja na sheria ya elimu ya mwaka 1978 vyombo ambavyo
ndivyo miongozo ya kuhakikisha watoto wanapata haki za msingi ikiwa ni pamoja
na elimu.
Mkuu wa mkoa ameitaka
jamii kuunga mkono juhudi za serikali katika kuboresha na kuimarisha
miundombinu iliyopo shuleni kwa kuchangia ujenzi wa nyumba bora za walimu na za
kutosha, kuongeza idadi ya madawati ili watoto wasikae chini, kuboresha hali ya
usafi wa mazingira ikiwepo idadi ya matundu ya vyoo kwa wasichana na wavulana,
upatikanaji chakula cha mchana kwa watoto wanapokuwa shuleni.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni