Na. Dajali Mgidange, IRINGA
Wananchi wa manispaa ya
Iringa wameaswa kutokuwatumikisha watoto katika ajira mbaya na unyanyasaji wa
aina yoyote ili watoto waweze kuishi katika amani na ukuaji stahiki.
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Iringa, Amani Mwamwindi |
Kauli hiyo imetolewa na
mstahiki Meya wa Manispaa ya Iringa Amani Mwamwindi alipokuwa akizungumza na
wananchi wa manispaa ya Iringa na watoto waliojitokeza katika maadhimisho ya
siku ya mtoto wa Afrika yaliyofanyika katika uwanja wa Mwembetogwa uliopo kata
ya Makorongoni manispaa ya Iringa.
Mwamwindi amewataka
wananchi wa manispaa ya Iringa kupinga utumikishaji wa watoto katika ajira
mbaya na hatarishi. Maeneo mengine hatarishi ameyataja kuwa ni mauaji ya
albino, ubakaji, ulawiti, vipigo na wazazi kutelekeza watoto wao.
“Maadhimisho haya hufanyika
kila mwaka kwa lengo la kuikumbusha jamii haki za watoto. Tukio hili ni kubwa
lina umuhimu wake katika manispaa yetu, Taifa na Kimataifa tukio hili ni
kumbukumbu ya watoto wapatao 15,000 waliouwawa na makaburu huko Soweto Afrika
Kusini tarehe 16/06/1976 wakipinga maamuzi ya serikali hiyo kuwafundisha watoto
lugha ya kikaburu” alisema Mwamwindi.
Akiongelea kaulimbiu ya
maadhimisho isemayo kupata elimu bora isiyo na vikwazo ni haki ya kila mtoto,
Meya amesema kuwa kaulimbiu hiyo imesisitiza
wazazi, walezi, familia,
serikali na wadau mbalimbali wanaojishughulisha na shughuli za maendeleo ya
watoto kwa kuliangalia kundi hili, kuhakikisha wanapata haki zao za msingi za
kupata elimu bila vikwazo kwa msingi kwamba mtoto awapo shuleni hatakiwi
kunyanyaswa kwasababu haki yake yeye ni kusoma na kupata Elimu. Amesema kuwa masuala
ya ada, michango mbalimbali ni jukumu la mzazi au mlezi. Amesema kuwa kumekuwepo
na tabia ya baadhi ya watoto kurudishwa nyumbani kwa kisingizio cha
kutokumaliza ada na baadhi ya michango
na kusisitiza kuwa jukumu hilo ni la mzazi.
Regina Mushi ambaye ni
mzazi alisema siku ya mtoto wa Afrika ni
siku nzuri kwa watoto kwa sababu imeweza kuwakutanisha pamoja na kujadili
changamoto zinazowakabili. Amesema kuwa imekuwepo changamoto ya baadhi ya
wazazi/ walezi kuwafungia watoto ndani na mwingine aliweza kumfungia mtoto
kwenye boksi na hatimae baadae kufariki.
Mtoto Henry Mwalongo amesema
“siku ya mtoto wa Afrika inawahimiza wazazi kutowanyanyasa watoto hasa katika
swala la elimu kutupatia elimu isiyo na vikwazo vya aina yoyote ile”.
Siku ya mtoto wa Afrika kuadhimishwa
tarehe 16 Juni kila mwaka barani Afrika kufuatia mauaji ya watoto zaidi ya
15,000 huko Soweto Afrika Kusini.
=30=
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni