Na. Frank Kibiki- KILOLO
WATANZANIA
wametakiwa kuwapuuzia na kutowafuata wanasiasa wachache wenye uchu wa madaraka
na nia ya kuvuruga mchakato wa kupata katiba mpya, unaeondelea hapa
nchini.
Kiongozi wa
mbio za Mwenge, Rahel Kassanda alitoa wito huo wilayani Kilolo, mkoani Iringa
wakati akizungumza na wakazi wa wilaya hiyo juu ya ujumbe wa mwenge wa uhuru
kwa mwaka huu, unaohamasiaha wananchi kushiriki katika mchakato huo.
Kassanda
alisema wapo baadhi ya wanasiasa wachache ambao wameonekana wazi wakitaka
kuvuruga mchakato wa katiba mpya, ambao Rais Jakaya Kikwete aliuasisi ili
kuhakikisha katiba hiyo ambayo kwa mara ya kwanza imeshirikisha wananchi,
inapatikana.
“Wapuuzeni hawa
wanasiasa wachache ambao wanaonekana wakitaka kuvuruga mchakato wa katiba mpya
kwa maslahi yao wenyewe, achaneni nao nanyi mjitokeze kupiga kura mara zoezi
hili litakapokuwa tayari, Tanzania sasa tunahitaji katiba mpya,”alisema.
Awali mkuu wa mkoa wa Iringa,
Dk Christine Ishengoma alitoa wito kwa wananchi wa mkoa huo kujiandaa na zoezi
la kupiga kura ya maoni ya rasimu ya katiba mpya wakati muda utakapofika, ili
watumie ipasavyo haki yao ya msingi kikatiba.
Akipokea Mwenge
wa uhuru aliokabidhiwa na Mkuu wa mkoa wa Morogoro, Joel Bendera Dk Ishengoma
alisema ni wajibu wa kila mkazi wa mkoa huo kutumia haki hiyo kikatiba.
“Ujumbe huu ni
muhimu sana hasa katika kipindi hiki ambacho watanzania tunapaswa kushikamana
zaidi na kuwa wamoja tunapoelekea katika kukamilisha mchakato wa kupata katiba
mpya, ambayo itakuwa dira ya kuliongoza taifa hili sasa na miaka ijayo,”alisema
Dk Ishengoma.
Alisema katika
kuhakikisha wananchi wa mkoa huo wanashiriki kikamilifu kwenye mchakato wa
katiba mpya, serikali inashirikisha wadau wengine kuendelea kutoa elimu kwa
jamii ili ione suala hilo linawahusu moja kwa moja.
Dk Ishengoma
aliwataka wananchi wa mkoa huo kuendelea kudumisha amani, utulivu na mshikamano
ikiwa ni pamoja na kuepukana na tabia ambazo zinaweza kuhatarisha mambo hayo.
“Wananchi wa
Iringa wanaimani kubwa kwamba sasa watapata katiba mpya, ambayo italiongoza
taifa kwa miaka mingi ijayo, huku dira ikiwa kuendelea kuwa na taifa
imara,”alisema mkuu huyo wa Mkoa.
Alisema Mwenge
huo ukiwa mkoani Iringa, utazindua miradi 42 yenye thamani ya zaidi ya sh
bilioni 3.1.
Aliitaja miradi
hiyo kuwa ni ya sekta za kilimo, barabara, elimu, afya, maji na maendeleo ya
jamii vikiwemo vikundi vya kiuchumi.
Mwisho.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni