Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa - IRINGA
Wakuu wa Mikoa ya Nyanda za Juu
Kusini watakiwa kudumisha amani na usalama ili kuvutia uwekezaji endelevu kwa
lengo la kukuza uchumi na kipato cha mtu mmojammoja.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri Mkuu
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mizengo Pinda alipokuwa akifungua Kongamano
la uwekezaji Nyanda za Juu Kusini lililofanyika leo jijini Mbeya.
Pinda amesema kuwa hakuna uwekezaji
endelevu na wenye tija katika maeneo yenye fujo, vurugu na uvunjifu wa amani.
Amesema kuwa uwekezaji wenye tija mara zote hufanyika katika maeneo yenye
utulivu mkubwa na amani. Aidha, ameutaka uongozi wa mikoa hiyo kutoa nafasi
kubwa ya ushirikiano baina ya sekta binafsi na sekta ya umma kutokana na
umuhimu wao katika kuleta maendeleo.
Akiongelea umuhimu wa kongamano hilo,
Waziri Mkuu amesema kuwa lengo la
kongamano hilo ni kuibua fikra mpya za mikoa na kanda kujiamini kuwa wanauwezo
wa kuvuta fursa za uwekezaji na kukuza uchumi, kuongeza pato la taifa na
kupambana na umasikini kwa wananchi. Amesema kuwa wawekezaji wameanza kuona Dar
es Salaam si mahali pekee pa kuwekeza tatizo wanalokumbana nalo hawajapata
taarifa za maeneo yenye fursa za uwekezaji.
Waziri Mkuu ameitaka kanda hiyo
kujipanga vizuri katika kilimo cha mbogamboga na matunda kwa lengo la kuinua
pato la mikoa hiyo.
Akiongelea kilimo cha mahindi, Waziri
Pinda amesema kuwa nchi ya Tanzania ni ya tano katika Afrika kwa uzalishaji wa
mahindi ikishika nafasi ya 15 duniani. Ameitaja changamoto kuwa Tanzania ni nchi
ya mwisho katika makundi yote mawili katika tija na kuitaka mikoa hiyo kuongeza
tija katika kilimo cha mahindi na usindikaji wake. Aidha, ameitaka mikoa hiyo
kujipanga kimvuto wa viwanda vya mbolea ili kuhakikisha mbolea inakuwepo ya
kutosha na kwa gharama za kawaida.
Akiongelea sekta ya mifugo katika
ukanda huu, Waziri Mkuu amesema kuwa wakati kanda hiyo ikijivunia wingi wa
mifugo ikiwa na ng’ombe zaidi ya
1,000,000 na mbuzi zaidi ya 500,000 inakabiliwa na changamoto ya viwanda vya usindikaji
nyama. Aidha, amemuagiza Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu- Dkt. Mary Nagu
kuhakikisha kiwanda cha kusindika nyama cha Mbeya kinaanza kazi mara moja kwa
kuwataka wadau wote kukaa pamoja na kutoka na suluhisho.
Waziri Mkuu amewahakikishia
wawekezaji umeme wa uhakika. Amesema kuwa serikali imejipanga kuwa na umeme wa
kutosha nchini ifikapo mwaka 2015. Amezitaka mamlaka za serikali za mitaa
kuondoa umangimeza na vikwazo visivyo vya lazima katika kuhamasisha uwekezaji. “Msiwe
kikwazo, kuweni wawezeshaji. Ninyi si watawala ni waleta maendeleo katika
jamii” alisisitiza Waziri Mkuu.
Kongamano la uwekezaji kwa mikoa ya
Iringa, Njombe na Mbeya ni muitikio wa agizo la Waziri Mkuu, Mizengo Panda
kuhakikisha makongamano yanafanyika katika ngazi ya kanda ili kuweza kuvutia
wawekezaji nchini kwa lengo la kukuza uchumi nchini.
MWISHO
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni