Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa- IRINGA
Mkoa wa Iringa umewaalika wawekezaji
kuwekeza katika sekta ya kilimo pamoja na sekta nyingine ili kuinua uchumi wa
wananchi wake.
Mualiko huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa
wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma alipokuwa akitoa neon la ufunguzi katika
kongamano la uwekezaji kwa mikoa ya Iringa, Njombe na Mbeya lililofanyika
katika ukumbi wa Mkapa jijini Mbeya.
Dkt. Ishengoma amewataka wawekezaji
kutumia fursa za uwekezaji katika kilimo. “Kilimo ni muhimu na muhimili mkuu
ukitoa ajira kwa asilimia 85. Hali ya hewa kwa ustawi wa mazao ya chakula na
biashara na ufugaji” alisisitiza Dkt. Ishengoma. Amesema kuwa msisitizo ni
uwekezaji katika kilimo cha umwagiliaji. Ameyataja mazao makuu yanayolimwa
Iringa kuwa ni mahindi, mpunga, maharage, ndizi, maua na matunda. Aidha,
amesisitiza kuwa mazao yote yanastawi katika mkoa wa Iringa.
Mkuu wa Mkoa amekaribisha uwekezaji
katika sekta za elimu na afya. Amesema kuwa pamoja na jukumu lililofanywa na
serikali katika kuwekeza kwenye sekta za elimu na afya bado uwekezaji
unahitajika katika maeneo ya miundombinu hasa ujenzi wa maabara na mabweni.
Maeneo mengine ni ujenzi wa miundombinu ya afya na huduma za afya kwa ujumla
wake. Amesema pia fursa ipo katika ujenzi wa vyuo vya uuguzi na udaktari katika
mkoa wa Iringa ili kusaidia kukabiliana na upungufu wa wataalamu katika fani
hizo.
Dkt. Ishengoma amesema kuwa pamoja na
mkoa kujivunia mtandao mzuri na imara wa barabara kwa ajili ya kusafirisha
mazao na malighafi mbalimbali, mkoa bado unahitaji wawekezaji katika viwanda
vya usindikaji mazao na matunda.
=30=
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni