Jumamosi, 17 Januari 2015

RC MASENZA ASEMA MAPINDUZI YA ZANZIBAR NI UKOMBOZI DHIDI YA WANYONGE



Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Mapinduzi matukufu ya Zanzibar ni ukumbozi dhidi ya wanyonge na utawala wa kisultani na kufurahia uhuru wa kweli kwa wananchi wa Zanzibar.

Kauli hiyo imetolewa na mgeni rasmi katika kumbukumbu ya maadhimisho ya Mapinduzi matukufu ya Zanzibar Amina Masenza wilayani Mufindi yalipofanyika maadhimisho ya kimkoa.

Masenza ambaye ni mkuu wa Mkoa wa Iringa amesema, “leo tunaadhimisha Kumbukumbu ya Miaka 51 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya Januari 12, 1964. Uwepo wenu hapa unadhihirisha jinsi sote kwa pamoja tunavyothamini na kuona umuhimu wa Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar. Tunapoadhimisha kumbukumbu hii ni vizuri mkafahamu kuwa Mapinduzi haya ndiyo yaliyowakomboa wanyonge kutokana na dhulma na kutawaliwa na kuwaletea Uhuru wa kweli wananchi wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.” Amesema kuwa mapinduzi hayo ndiyo msingi wa utu na heshima kwa wananchi na Taifa kwa ujumla. 

Ameongeza kuwa mapinduzi hayo yaliondoa aina zote za ubaguzi na kujenga misingi ya haki na usawa kwa watu wote. Amesema kuwa katika kipindi cha miaka 51 ya Mapinduzi matukufu ya Zanzibar mshikamano na uelewano miongoni mwa jamii umeendelea kujengeka na kuwa imara zaidi.

Akiongelea maadhimisho hayo katika mkoa wa Iringa, Mkuu wa mkoa amesema kuwa mkoa wake umeamua kuadhimisha Kumbukumbu ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar kwa shughuli ya upandaji miti. Amesema “sote tunatambua umuhimu wa miti katika maisha yetu. Mkoa umeona ni muhimu kutumia maadhimisho haya kuwakumbusha wananchi umuhimu wa kutunza mazingira hasa upandaji wa miti, ulindaji na utunzaji wa vyanzo vya maji.”

Amesema “napenda kuwakumbusha kuwa upandaji miti na usafi wa mazingira ni utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2010. Ilani hiyo inaelekeza umuhimu wa kutunza vyanzo vya maji na kuhamasisha usafi wa mazingira.”

Mkuu wa wilaya ya Mufindi, Evarista Kalalu amesema kuwa kumbukumbu hiyo ya Mapinduzi matukufu ya ya Zanzibar itumike kutafakari nwebendo wa jamii kuanzia ngazi ya familia hadi taifa katika kulinda Mapinduzi hayo kwa kizaji kilichopo na kizazi kijacho.

Mwisho, akitoa shukrani kwa hotuba ya mgeni rasmi, Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Mufindi, Peter Tweve amesema kuwa hotuba hiyo imewasaidia wananchi wa wilaya ya mufindi na mkoa wa Iringa kwa ujumla kukumbuka wajibu wao katika masuala ya msingi. Ameyataja masuala hayo kuwa ni elimu, afya, lishe, ujenzi wa maabara na ulinzi na usalama.
=30=


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Habari zinazoendelea hivi sasa

SERIKALI KUWEZESHA VIJANA KUKOPA

Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Iringa Serikali itaendelea kuwawezesha vijana kwa kuwatengenezea mazingira mazuri ya mikopo ili waweze k...