Jumamosi, 17 Januari 2015

WAVAMIZI UWANJA WA NDEGE WA IRINGA WAONYWA



NA TUMAINI MSOWOYA, IRINGA
SERIKALI imewaagiza watendaji wanaosimamia uwanja wa Ndege wa Nduli, uliopo manispaa ya Iringa kuzuia haraka wananchi walioanza kuvamia eneo hilo na kujenga makazi.

Baadhi ya wananchi wa manispaa ya Iringa, wamevamia eneo la uwanja wa ndege wa nduli na kujenga makazi, jambo litakalotishia urukaji na utuaji wa ndege na kuzuia upanuzi wa uwanja huo.

Akizungumza na watendaji hao, wakati wa ziara yake mkoani Iringa, Waziri wa uchukuzi Dr Harisson Mwakyembe alisema serikali ipo katika harakati za ukarabati wa viwanja vya ndege, hivyo ni jukumu la watendaji kusimamia maendeleo ya viwanja hivyo.

“Mpaka watu wanavamia na kuanza makazi nyie mnakuwa wapi? Kwanini mnakaa na taarifa za aina hii kwenye vitabu vyenu wakati serikali ipo na hatua zinapaswa kuanza kuchukuliwa?, zimamieni haraka kuzuia jambo hili,”alisema Dk Mwakyembe alisema lengo la kutembelea uwanja huo ni kuona namna mchakato wa ukarabati wake utakavyokuwa ili kuongeza hadhi ya viwanja vya ndege nchini kwa kuufanya usafiri wa anga, kutumika kwa nguvu tofauti na sasa.

Alimuomba mkuu wa Mkoa wa Iringa, kusaidia uzuiaji wa  kasi ya wananchi kuanza kujenga makazi ndani ya uwanja huo jambo ambalo, linaweza kusitisha zoezi la upanuzi wa uwanja. “Sasa kama uwanja huu utakuwa na migogoro maana yake muda wa utatuzi wa migogoro utasababisha jambo la ukarabati kuchelewa huku viwanja visivyo na matatizo ya aina hii vikifanyiwa kwa haraka, simamieni jukumu lenu na serikali itawasaidia mkijiweka wazi,”alisema 

Alisema uwanja wa ndege wa Iringa ukikarabatiwa utaweza kuongeza idadi ya abiria wa usafiri wa anga, ikiwa ndege kubwa zitaanza kutua.
Alisema kutokana na mkoa wa Iringa kuwa na vivutio vingi vya kitalii, uwanja wa ndege wa nduli utachangia kuongezeka kwa mapato ndani ya mkoa huo.

Aidha aliiagiza mamlaka ya viwanja nya ndege nchini, kuhakikisha kuwa uwanja huo unanunua gari la zimamoto kwa madai kuwa ni aibu kwa uwanja kukosa kwa huduma hiyo. Mbali na huduma ya zimamoto, alisema jambo lingine la msingi ni kuwepo kwa uzio ili kupunguza uvamizi wa wananchi kwenye eneo hilo.

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Msenzi alisema atatekeleza kwa vitendo agizo la kuhakikisha eneo hilo linalindwa bila kuvamiwa na watu. “Ninaanza kutekeleza jambo hili leo, nawaagiza manispaa ya Iringa kufanya tathmini haraka ili tujue nani amevamia na nani yupo nje,”alisema

Alisema katika tathmini hiyo, lazima kuzuia nyumba zote ambazo zipo kwenye ujenzi na zile ambazo zilijengwa siku nyingi zifahamike ili wananchi wawekwe kwenye orodha ya fidia wakati wa ukarabati utakapofika.

Akisoma taarifa ya uwanja huo wa Ndege, Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya viwanja vya ndege nchini, Thomas Haule alisema miongoni mwa changamoto zinazoukabiri uwanja huo ni watu kuvamia na kujenga makazi.

Alisema pia kuna eneo ambalo linahitaji fidia ya makazi katika mpango wa upanuzi abapo usanifu wa kina utaweka barabara ya kuingia na majengo mapya ya abiria na maegesho ya ndege. Aliitaja changamoto nyingine kuwa ni pamoja na uchakavu wa barabara ya kutua na kurukia ndege ambayo inahatarisha usalama wa ndege zinazotua kwenye uwanja huo.

Aidha aliongeza kuwa kutokuwepo kwa uzio wa usalama, vifaa vya ukaguzi wa usalama na gari la zimamoto kunachangia kupunguza hadhi ya uwanja huo. 

Kwa upande wake Meneja wa uwanja huo, Ana Kibona alisema pamoja na changamoto zinazoukabili uwanja huo, wamefanikiwa kuongeza safari za ndege kutoka 172 mwaka 2009  hadi 771 mwaka huu.

Hata hivyo alisema mwezi Mei mwaka huu, wanategemea kukamilisha mradi wa upembuzi yakinifu wa kina kwa viwanja 11 vya ndege katika mikoa mbalimbali hapa nchini.
Alisema ripoti ya upembuzi na makabrasha yatatumika kutafuta fedha za kazi za ukarabati na upanuzi katika viwanja husika ili kuinua sekta ya usafiri wa anga hapa nchini.
=30=

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Habari zinazoendelea hivi sasa

SERIKALI KUWEZESHA VIJANA KUKOPA

Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Iringa Serikali itaendelea kuwawezesha vijana kwa kuwatengenezea mazingira mazuri ya mikopo ili waweze k...