Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Ushiriki hasi wa jamii juu ya
utunzaji wa barabara ni kichocheo kikubwa cha uharibifu wa barabara mkoani Iringa.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa
wa Iringa, Amina Masenza alipokuwa akifungua kikao cha bodi ya barabara Mkoa wa
Iringa kilichofanyika katika ukumbi wa Siasa ni Kilimo mjini Iringa.
Masenza amesema “katika kuhakikisha
tunakuwa na barabara zinazopitika muda wote, nimeona mapungufu ya ushiriki wa
jamii juu utunzaji wa barabara hizo. Wananchi wamekuwa wakifanya shughuli ndani
ya hifadhi ya barabara na kuacha uchafu kwenye barabara na uchafu huo kuziba
mifereji na kuharibu barabara hizo hasa kipindi hiki cha mvua.” Amezitaka mamlaka
husika kuendelea kutoa elimu kwa wananchi ili washiriki kikamilifu katika
utunzaji wa barabara hizo kutokana na kuwa na manufaa kwa wananchi wote. Amesema kuwa
barabara hizo zimeendelea kuwa muhimu hasa kwa wakulima kuwezesha kusafirisha
mazao yao haraka na unafuu kuyapeleka sokoni.
Akiongelea kipindi hiki cha mvua,
Mkuu wa Mkoa amesema kuwa kipindi hiki jamii inakabiliwa na changamoto lukuki yakiwemo maafa yanayosababishwa na mvua.
Amezitaka mamlaka husika kufuatilia na kurekebisha maeneo korofi ili barabara katika maeneo hayo ziweze
kupitika muda wote. Ameyataja maeneo yanayotakiwa kuangaliwa kwa umakini zaidi
kuwa ni matengenezo ya mifereji, makaravati na madaraja.
Aidha, amewataka
Wakala wa barabara Mkoa wa Iringa na Halmashauri kuwasimamia vizuru wakandarasi
ili wafanye kazi kwa umakini na uhakika mkubwa ili barabara ziweze kudumu. Vilevile, ametaka elimu iendelee kutolewa kwa
wananchi kutokujenga katika maeneo yenye uwezekano wa kupata mafuriko.
=30=
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni