Na. Ofisi ya
Mkuu wa Mkoa
Wananchi wa vijiji vya Nyanzwa na Igunda wamepongezwa kwa juhudi
kubwa za kuendeleza kilimo katika eneo linalozunguka skimu ya umwagiliaji ya
Nyanzwa.
Pongezi hizo zimetolewa na Waziri Mkuu Mhe. Mizengo Pinda baada ya
kukagua skimu hiyo iliyopo katika Wilaya ya Iringa.
Mhe. Pinda amesema “nawapongeza wakulima na wananchi wa Nyanzwa na
Igunda kwa juhudi kubwa za kuendeleza kilimo katika eneo hilo. Nitoe wito kwa
uongozi wa kata na vijiji vya Nyanzwa na Igunda kuendelea kutunza chanzo cha
maji ya umwagiliaji katika skimu ya Nyanzwa”. Amewataka kushirikiana na uongozi
wa Halmashauri kuweka mipaka ya chanzo cha maji na kuweka utaratibu endelevu wa
kukitunza.
Amesema historia inaonesha kuwa chanzo cha maji cha Nyanzwa
kilikuwa na uwezo mkubwa wa kumwagilia hekta 940 na kuutaka uongozi wa Mkoa na
Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo kukaa na kuandaa mpango mahususi wa kuendeleza
skimu ya umwagiliaji na kufanya mapitio ya upembuzi yakinifu iliyofanyika awali
ili kuweza kuingiza mradi huo katika mpango na bajeti ya Halmashauri ya Kilolo
kwa mwaka 2015/2016.
Katika kutoa msukumu kwa wakulima kupata mitaji ya kilimo, Mhe.
Pinda alishauri Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo isaidie vijiji vya Nyanzwa na
Igunda kufufua jumuiya yao ya ushirika iliyokuwa inaundwa na vijiji vya
Nyanzwa, Igunda na Mgowelo au kuunda SACCOS mpya ambayo ni imara zaidi na
kuwataka Maafisa Ushirika wawasaidie wakulima kuunda chombo hicho.
Kutokana na hali ya kijiografia na fursa kubwa ya kuendeleza
ufugaji nyuki katika vijiji vya Nyanzwa na Igunda, Waziri Mkuu aliushauri
uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo kutazama uwezekano wa kuanzisha
mradi wa ufugaji nyuki kwa lengo la kuongeza kipato cha wananchi.
=30=
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni