Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Walimu nchini wametakiwa kuachana na
tabia za kuwakatisha tamaa watoto wa kike kujikita katika masomo ya sayansi kwa
kisingizio kuwa ni magumu.
Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa
Kampuni ya Rodhance, Upendo Kilale alipokuwa akiongea na mwandishi wetu katika
kilele cha maadhimisho ya siku ya wanawake duniani iliyofanyika katika uwanja
wa mashujaa mjini Mafinga.
Bi. Kilale amesema kuwa wapo
wasichana wengi wanaopenda kusoma masomo ya sayansi na kuonesha nia lakini
wamekuwa wakikatishwa tamaa na baadhi ya walimu wao kuwa masomo hayo ni magumu.
Amesema kuwa walimu wanalo jukumu kubwa la kuwatia moyo wasichana ili wasichana
wengi wajikite katika masomo ya sayansi. Aidha, ameitaka jamii kwa ujumla
kubadili mtazamo hasi kwa wasichana linapokuwa suala la masomo ya sayansi
nchini.
Bi. Kilale amesema kuwa mwanamke
aliyesoma masomo ya sayansi familia yake inakuwa na afya njema na hali bora ya
kimaisha. Akiongelea zaidi suala la kiafya, amesema kuwa mwanamke aliyesoma sayansi
anakuwa na uelewa mkubwa wa kuandaa chakula kwa kuzingatia uwiano wa makundi tofauti
ya vyakula. Ameyataja makundi hayo kuwa ni protini, wanga, mafuta na vitamin.
Amesema kuwa taifa katika kipindi hiki linakabiliwa na tatizo la lishe kutokana
na jamii kushindwa kufanya uwiano wa makundi ya vyakula katika kuandaa mlo.
Amesema kuwa ili kukabiliana na tatizo la lishe ni lazima wasichana ambao ni
wanawake watarajiwa waandaliwa sasa kwa kuwahamasisha kusoma masomo ya sayansi.
Amesema kuwa kampuni yake inalenga
kuifahamisha jamii kuwa wanawake wanaweza kufanya mambo mazuri katika masomo ya
sayansi na kuitumia sayansi katika kubadilisha maisha ya kila siku.
Kampuni ya Rodhance inamakao yake
makuu jijini Dar es Salaam ikiwa na tawi katika mji wa Mafinga mkoani Iringa.
=30=
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni