Na. Ofisi ya
Mkuu wa Mkoa
Waziri Mkuu Mhe. Mizengo Pinda amewapongeza wananchi wa Wilaya ya
Iringa kwa kazi nzuri ya ujenzi wa Vituo vya Afya kwa lengo la kuboresha afya
za wananchi wa Wilaya hiyo.
Kauli hiyo ameitoka Wilayani Mufindi alipokuwa akifanya majumuisho
ya ziara yake kwa kila Wilaya.
Mhe. Pinda amesema “naomba nitumie fursa hii kuwapongeza wananchi
wa Wilaya ya Iringa kwa kazi nzuri mnayoifanya katika ujenzi wa Vituo vya Afya”.
Ametolea mfano Kituo cha Afya cha Mlowa alichokitembelea na kukifungua rasmi
kuwa kitawapunguzia wananchi kero ya usafiri wa kwenda umbali mrefu kupata
huduma ya afya. “Ni rai yangu kuwa kituo hiki kitatumika na kutoa huduma kwa
wananchi wa Mlowa na majirani. Hakikisheni kituo hiki kinadumu” alisisitiza
Waziri Mkuu.
Mhe. Pinda hakusita kukipongeza kituo hicho kwa kutenga dirisha
maalum la kuhudumia wazee. “Nilipokuwa katika Kituo cha Afya cha Mlowa
nilifarijika kuona dirisha maalum la kuhudumia wazee wenye umri mkubwa kuanzia
miaka 60.” alisema Mhe. Pinda.
Ametumia nafasi hiyo kuwaasa viongozi wa Mkoa na Wilaya kuendeleza
utamaduni na sera hiyo nzuri ya kuwajali wazee. Amesema kuwa kutokana na wazee
kuwa wanakabiliwa na magonjwa ya kipekee yanayoendana na umri wao. Ameyataja
magonjwa yanayowakabili wanaume kuwa tatizo la shinikizo la damu na saratani ya
tezi dume lakini tatizo likijulikana mapema linatibika. Aidha, ameyataja
magonjwa yanayowakabili wanawake zaidi kuwa ni saratani ya mlango wa kizazi,
UTI, Fistula na Malaria. Wananchi wakielimishwa dalili za magonjwa hayo watakwenda
Kituo cha Afya mapema na hivyo kupunguza uwezekano wa kuugua kwa muda mrefu na
pengine kupoteza maisha. Amewataka viongozi kuwahamasisha wananchi kujenga
tabia ya kupima afya mapema ili kujua kuwepo kwa maradhi.
Waziri Mkuu, akiongelea skimu ya umwagiliaji ya Magozi, amesema
kuwa changamoto kubwa aliyoiona inayowakumba wananchi na vikundi vya wakulima
wa mpunga wa vijiji vya Mkombilenga, Ilolompya na Magozi ni njia bora ya
kutumia kwa tija zana bora za kilimo zilizopo kwa lengo la kuongeza uzalishaji.
Katika skimu hiyo Waziri Mkuu alimshauri Mkuu wa Mkoa kuwasiliana na Mkoa wa Morogoro
ili kujifunza namna kampuni ya mpunga ya Kilombero inavyoshirikisha wakulima
wadogo katika kilimo cha mpunga.
Aidha, aliwashauri kuungana na kutengeneza
vijishamba vyao katika mashamba makubwa ya pamoja ili opereresheni za kilimo
zifanyike kwa pamoja.
=30=
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni