Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Wasimamiaji wa mpango wa
kunusuru kaya masikini mkoani Iringa wametakiwa kuimarisha uwazi, uwajibikaji
na kuruhusu makundi tofauti kushiriki kwa kutumia mfumo madhubuti wa wanufaika.
Kauli hiyo imetolewa na
Mkuu wa mkoa wa Iringa, Amina Masenza katika hotuba yake ya ufunguzi wa warsha
ya kujenga uelewa wa wadau kuhusu mpango wa kunusuru kaya masikini TASAF awamu
ya III iliyofanyika ukumbi wa mikutano wa Valentine mjini Iringa na kusomwa na
Mkuu wa Wilaya ya Kilolo, Seleman Mzee.
Masenza alisema “ni mategemeo yangu kuwa utekelezaji wa
mpango huu wa kunusuru kaya masikini utaimarisha uwazi, uwajibikaji na kutoa
fursa kwa makundi mbalimbali kushiriki kwa kutumia mfumo madhubuti wa kubaini
walengwa katika vijiji na mitaa yetu”. Alisema muundo wa awamu ya tatu, umezingatia vema
changamoto ambazo zilijitokeza katika utekelezaji wa awamu ya pili. Alisema kwa
maana hiyo usimamizi na ufuatiliaji umeimarishwa katika ngazi ya mkoa,
halmashauri na kata kwa kuhusisha watumishi zaidi kufuatilia shughuli za mfumo
wa maendeleo ya jamii. “Napenda
kusisitiza azma ya serikali ya kuhakikisha kuwa wananchi wanapata maendeleo na
ndiyo lengo la kuanzisha mpango huu ambao utatekelezwa katika vijiji na mitaa
yetu ili kuondoa umasikini kwa manufaa ya jamii yetu” alisisitiza Masenza.
Akiongelea utekelezaji wa
mpango huo, mkuu wa mkoa alisema kuwa utekelezaji wa mpango huo unatarajiwa
kuwafikia wastani wa walengwa 6,500,000 katika kaya masikini na zilizo katika
mazingira hatarishi 1,000,000 za Tanzania. Alisema viongozi wanao wajibu wa
kusimamia vizuri mpango huo ili kuhakikisha kaya zilizotambuliwa na
kuandikishwa kwenye orodha ya kaya masikini, zinafaidika kwa kushiriki katika
program ya uhawilishaji fedha, program ya mradi ya ujenzi ambayo itatoa fursa
za ajira za muda katika kipindi cha hari, program ya kujenga uwezo wa kujikinu
na kuongeza kipato na kujengewa uwezo.
Mwakilishi wa mkurugenzi
mkuu wa TASAF, Richard Njalika alisema kuwa mpango wa kunusuru kaya masikini
umepangwa kutekelezwa kwa awamu ili kufikia jumla ya halmashauri 169 za
Tanzania. Awamu za utekelezaji mpango huu zimelengwa kujenga uwezo kwa
wawezeshaji wa kutosha na kujenga mifumo pamoja na kuboresha utekelezaji katika
kila awamu. Alisema kuwa awamu hii imepangwa kutekelezwa kwa kipindi cha miaka
10 katika awamu mbili za miaka mitano mitano. Alisema kuwa utekelezaji wa
mpango unahitaji uwekezaji mkubwa kwenye mifumo na kujenga uwezo katika ngazi
zote za utekelezaji.
Akiongelea sehemu za
mpango huo, mwakilishi wa mkurugenzi mkuu wa TASAF alizitaja sehemu hizo kuwa
ni kujenga uwezo katika ngazi zote za utekelezaji na kujenga na kuboresha
miundombinu inayolenga sekta za elimu, afya na maji. Seheumu nyingine ni
uhawilishaji fedha, ambapo unatoa ruzuku kwa kaya masikini sana zinazotambuliwa
kwa mchakato unaoshirikisha jamii. Kuongeza kipato kwa kaya masikini kupitia
uwekaji akiba na shughuli za kiuchumi ili kuboresha maisha. Eneo lingine ni
kutoa ajira kwa kaya masikini zenye watu wenye uwezo wa kufanya kazi wakati wa
hari.
=30=
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni