Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Wafanyakazi mkoani Iringa wametakiwa
kuzingatia miiko na maadili ya kazi katika utendaji kazi wao ili waweze
kuwatumikia wananchi vizuri.
Kauli hiyo ilitolewa na mkuu wa mkoa
wa Iringa, Amina Masenza alipokuwa akihutubia mamia ya wafanyakazi wa mkoa wa Iringa
katika kilele cha siku ya Mei Mosi kilichofanyika kimkoa mjini Mafinga.
Masenza alisema “kila kazi ina miiko yake, tunapodai mabadiliko lazima tuzingatie miiko
iliyopo. Lazima tufanye kazi, tuiheshimu kazi na tuwajibike ipasavyo. Lazima tuwe
na maadili ya kazi. Ili mfanyakazi yeyote aweze kuheshimika inampasa kuelewa
umuhimu wa nafasi yake katika jamii, kwa kufanya kazi kwa juhudi, weledi,
nidhamu na kwa malengo. Mfanyakazi usingoje kufuatwa fuatwa na msimamizi wako”.
Alisema kuwa wafanyakazi wanatakiwa kuelewa sheria za kazi na mahusiano kazini,
taratibu na kanuni za kazi, kuheshimu maadili na taaluma na kutunza siri za
ofisi kwa mujibu wa taratibu za ofisi na kuepuka upendeleo na ubaguzi katika
utoaji wa huduma kwa wananchi. Alisema kuwa kuyafanya mambo hayo, wafanyakazi
watakuwa wakienzi na kuitetea dhana ya mabadiliko kuinua hali ya wafanyakazi.
Akiongelea vyama vya wafanyakazi,
mkuu wa mkoa alisema kuwa vyama vya wafanyakazi vinawajibu mkubwa kuhakikisha ustawi
wa wafanyakazi na waajiri. Vilevile, alivitaka vyama kuwaelimisha wafanyakazi
wa serikali na binafsi kuheshimu nafasi walizopewa katika jamii na kuelewa
misingi ya utumishi bora kwa umma.
Aidha, alivitaka kushirikiana na waajiri
kutatua kero zinazowakabili wafanyakazi. “Vyama vya wafanyakazi kamwe visifuge
uzembe, wizi na utapeli unaojitokeza” alisisitiza mkuu wa mkoa.
“Waajiri
mnawajibu mkubwa wa kuhakikisha kazi zinafanywa kwa ufanisi, mshikamano na
uadilifu. Mnapaswa kutoa vitendea kazi bora, kujali usalama wa wafanyakazi na
kutoa ushirikiano wa kutosha kwa wafanyakazi” alisisitiza Masenza.
Aliongeza kuwa uhai wa taasisi unategemea sana uwepo wa wafanyakazi na kuwataka
kutambua umuhimu wa wafanyakazi na kuwapa motisha.
Katika risala iliyosomwa na mratibu
wa TUCTA mkoa wa Iringa, Deus Waileta alisema kuwa maboresho ni muhimu katika
mfumo wa hifadhi ya jamii. Alisema kuwa mifuko isiyojiendesha vizuri na kufanya
uwekezaji usio na tija na maslahi kwa wananchama ichunguzwe. Aliiomba serikali
kusimamia suala la kima cha chini cha mshahara kwa taasisi zote ili kuwe na
uwiano sawa kwa wafanyakazi wote. Mambo mengine aliyoyawasilisha ni baadhi ya
waajiri kukaidi kuchangia mifuko ya hifadhi ya jamii na mishahara midogo kwa
wafanyakazi na wengine kutokupewa mikataba ya ajira.
Maadhimisho ya sherehe za Mei mosi
mwaka 2016 kitaifa zilifanyika mkoani Dodoma zikiongozwa na kauli mbiu isemayo
‘dhana ya mabadiliko ilenger kuinua hali ya wafanyakazi’.
=30=
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni