Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Wakurugenzi
wa mamlaka za serikali za mitaa mkoani Iringa wameagizwa kuwasimamia watumishi
walio chini yao ili watekeleze majukumu yao kwa kufuata maadili ya utumishi wa
umma na misingi ya utawala bora.
Agizo
hilo lilitolewa na Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Wamoja Ayubu alipokuwa
akifungua semina ya siku mbili kwa viongozi wa mamlaka za serikali za mitaa
mkoani hapa iliyoandaliwa na Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma na
kufanyika katika ukumbi wa Veta mjini Iringa.
Ayubu
alisema “natumia semina hii kuwaagiza
wakurugenzi wa mamlaka za serikali za mitaa wote mkoani Iringa kuwasimamia
ipasanyo watumishi wote walio chini ya mamlaka zenu ili waweze kutimiza wajibu
wao kwa kufuata maadili ya utumishi wa umma na misingi ya utawala bora”.
Aliongeza kuwa kufanya kazi kwa kufuata maadili ya utumishi wa umma na misingi
ya utawala bora kutamuhakikishia mwananchi kupata huduma bora na kuondoa
malalamiko ya kiutendaji kwa watumishi wa serikali.
Alisema kuwa mabadiliko katika sekta ya umma yanaendelea
kufanyika katika taasisi zote za umma kwa msisitizo wa kufuata kanuni na
maadili ya utumishi wa umma kwa viongozi wa umma na watumishi wa umma. “Mabadiliko haya yanalenga kubadilisha dhana
iliyozoeleka ya kufanya kazi kwa mazoea pasipo kufuata misingi ya utawala bora
na utawala wa sheria. Hivyo, dhana ya maadili ya utumishi wa umma inahitaji
sana ushiriki wetu sote kama viongozi na washiriki wa semina hii. Mabadiliko ya
kiutendaji kazi katika sekta ya umma yatategemea sana utendaji wa viongozi na
watumishi hasa wa serikali za mitaa kwa sababu ndiyo walio karibu zaidi na
wananchi. Hivyo, rai yangu kwenu ni kufanya kazi kwa kuzingatia maadili,
misingi ya utumishi wa umma, utawala bora na kufuata utawala wa sheria”.
Akiongelea
Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015 inayotekelezwa na serikali ya awamu ya
tano ibara ya 148 (e) inasisitiza kuimarisha ubora na upatikanaji wa huduma za
kijamii ambazo ni afya, elimu, maji na miundombiny ya kiuchumi katika
halmashauri. Aidha, sehemu (f) inataka serikali kuchukua hatua kali za
kinidhamu na kisheria dhidi ya watendaji wa halmashauri za wilaya
watakaobainika kuhusika na vitendo vya ubadhirifu na wizi wa mali ya umma
pamoja na matumizi mabaya ya madaraka.
Katibu Tawala Mkoa alisisitiza “nimeona niyakumbushe haya kwa sababu
utendaji kazi wa viongozi wa mamlaka za serikali za mitaa unajikita katika
kusimamia na kutekeleza mambo haya. Na kwa kuzingatia misingi ya maadili
iliyoainishwa katika ibara ya 132 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
ya mwaka 1977 na masharti ya sheria ya maadili ya viongozi wa umma Na. 13 ya
mwaka 1995, yanayomtaka kila kiongozi wa umma kuzingatia viwango vya juu vya
maadili ili kukuza utu, uwazi, uadilifu, uwajibikaji na kuimarisha imani ya
wananchi kuhusu utendaji wa serikali yao’’.
Sekretarieti
ya Maandili ya Viongozi wa Umma iliandaa semina hiyo kwa lengo la kuwajengea
uwezo na uelewa mpana viongozi wa Serikali za Mitaa katika Mkoa wa Iringa ili
waweze kutekeleza vizuri majukumu yao ya kila siku kwa mujibu wa sheria
inayosimamia maadili ya viongozi wa umma, sheria ya maadili ya viongozi wa umma
Na. 13 ya Mwaka 1995 chini ya kaulimbiu ‘tuzingatie maadili kwa maendeleo ya
taifa’.
=30=
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni