Na.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Makampuni ya ulinzi mkoani Iringa yametakiwa kuwatumia
askari wastaafu kutoka majeshi ya ulinzi kwa mujibu wa sheria ili kunufaika na
ujuzi walionao na kuimarisha usalama wa nchi.
Kauli hiyo ilitolewa na mkuu wa mkoa wa Iringa, Amina
Masenza alipokuwa akifungua mkutano mkuu wa chama cha makampuni binafsi ya
ulinzi mkoa wa Iringa (TSIA) kilichofanyika katika bwalo la Polisi mjini Iringa
jana.
Masenza alisema “wito wangu
kwenu ni kwamba
hakikisheni wasimamizi wa makampuni ya ulinzi wanakuwa wastaafu kutoka majeshi
ya ulinzi kwa mujibu wa sheria. Wastaafu hawa wanauzoefu na ujuzi katika
kusimamia masuala yote ya kiulinzi na usalama”. Aliongeza kuwa wastaafu hao
wanauwezo wa kudhibiti nidhamu na kufundisha maadili mema kwa walinzi. Alisema
kuwa walinzi wengi katika makampuni hayo wanakabiliwa na tatizo la nidhamu na
maadili hivyo kuwatumia askari wastaafu kutawasaidia kuimarisha nidhamu na
maadili kwa walinzi wa makampuni hayo.
Mkuu wa mkoa wa Iringa alipongeza juhudi zinazofanywa
na makampuni ya ulinzi mkoani hapa. Alisema “mimi binafsi nichukue nafasi hii kutambua juhudi mbalimbali
zinazofanywa na makampuni ya ulinzi katika kuimarisha hali ya amani miongoni
mwa jamii na taasisi mbalimbali. Makampuni ya ulinzi yana mchango mkubwa katika
kulinda mali za raia wa Tanzania. Pasingekuwepo makampuni haya vyombo vyetu vya
ulinzi haviwezi kulinda peke yao kwa kuwa watanzania ni wengi na askari ni
wachache lakini pia mali za watanzania ni nyingi na ukizingatia wahalifu
wanaongezeka na kubuni mbinu mpya kila kukicha”.
Mkuu wa mkoa wa Iringa ambaye pia ni mwenyekiti wa
kamati ya usalama ya mkoa aliagiza makampuni yote ya ulinzi mkoani Iringa
kuhakikisha walinzi wake wote wanapitia mafunzo ya JKT au mgambo. “Walinzi wanapaswa kupitia mafunzo ya JKT au
mgambo. Mafunzo haya huwajengea uwezo wa kupambana na majambazi, kuzuia matendo
ya kihalifu na kulitumikia Taifa kizalendo” alisisiza mkuu wa mkoa.
Awali afisa upelelezi
mkoa wa Iringa, Deusdedit Kasindo waliwakumbusha wamiliki wa makampuni ya ulinzi
kuwa ni wabia wa jeshi la Polisi kwa sababu wanafanya kazi zinazofanana za
kulinda raia na mali zao. Alisisitiza kuwa viongozi wa makampuni hayo
wanatakiwa kuwa na taaluma ya ulinzi na walinzi wao wanatakiwa kuwa na taaluma
ya ulinzi.
Kasindo aliwakumbusha wamiliki wa makampuni ya ulinzi
kuwa wanatakiwa kuwa na silaha mbili angalau tofauti na maeneo mengi ambayo
walinzi wanakuwa na silaha moja jambo ambalo ni rahisi kuvamiwa. Aliwakumbusha
kuwa kuazima silaha ni kosa kisheria. Aidha, aliwataka wamiliki wa makumpuni
hayo kuhakikisha walinzi wao wanajua kutumia silaha kikamilifu.
=30=
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni