Jumapili, 23 Julai 2017

IRINGA GIRLS YADHIBITI NIDHAMU



Na Mwandishi Maalum Iringa
Shule ya sekondari ya wasichana Iringa imefanikiwa kudhibiti nidhamu kwa walimu na wanafunzi katika juhudi za kujenga mazingira mazuri ya kufundishia na kujifunzia.

Kauli hiyo ilitolewa na mkuu wa shule ya sekondari ya wasichana ya Iringa, mwalimu Blandina Nkondola alipokuwa akiwasilisha taarifa ya shule kwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia alipotembelea shule hiyo katika ziara ya kikazi hivi karibuni.

Mwalimu Nkondola alisema “shule yetu imefanikiwa kusimamia suala la nidhamu kwa wanafunzi na walimu mpaka sasa hali ni tulivu japo kuna changamoto ndogondogo ambazo tunaendelea kukabiliana nazo na kuzitafutia ufumbuzi’’. 

Akiongelea uelewa wa haki za wanafunzi, alisema kuwa wanafunzi wamekuwa na uelewa mkubwa sana juu ya haki zao. “Wanafunzi wamekuwa na uelewa mkubwa sana juu ya haki zao pamoja na suala zima la rushwa na hasa rushwa ya ngono ambayo awali lilikuwa ni tatizo. Hii inatokana na elimu ambayo wamekuwa wakiipata mara kwa mara kutoka kwa uongozi wa shule” alisema mwalimu Nkondola.

Akiongelea changamoto za kielimu, mkuu huyo alizitaja kuwa ni ukosefu wa semina za mara kwa mara za lugha za alama kwa walimu wanaofundisha lugha za alama. Changamoto nyingine aliitaja kuwa ni uchache wa wakalimani wa masomo ya sayansi na walimu wa hisabati, fizikia na chakula na lishe.

Akiongelea mafanikio ya kiutawala, mkuu wa shule alisema kuwa shule yake imefanikiwa kutokuzalisha madeni mapya kwa mwaka wa fedha 2016/2017. Alisema kuwa shule yake imefanikiwa kukarabati mfumo wa umeme na kuchimba kisima cha maji na kuondoa tatizo la kukatika umeme mara kwa mara na maji kutokana na fedha zilizotolewa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia shilingi milioni 60.

Akiwa shuleni hapo, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalachako alisema kuwa wizara yake itahakikisha walimu wa lugha za alama wanapatiwa mafunzo ili waweze kutekeleza majukumu yao kikamilifu. Aidha, aliupongeza mkoa kwa kusimamia suala la nidhamu katika shule hiyo.
=30=





Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Habari zinazoendelea hivi sasa

SERIKALI KUWEZESHA VIJANA KUKOPA

Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Iringa Serikali itaendelea kuwawezesha vijana kwa kuwatengenezea mazingira mazuri ya mikopo ili waweze k...