Na. Dennis Gondwe, Iringa
Walimu nchini
wametakiwa kuwa wavumilivu na kuendelea kuchapa kazi na kuiamini Serikali
inayoongozwa na Rais Dk. John Magufuli kuwa italipa madeni yao kwa mujibu wa
taratibu za nchi.
Kauli hiyo
ilitolewa na waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako
alipokuwa akiongea na walimu na jumuiya ya shule ya sekondari ya wasichana ya Iringa
alipofanya ziara ya kikazi mkoani Iringa na kutembelea shule hiyo juzi.
Prof. Ndalichako
alisema kuwa Serikali inatambua kuwa walimu wanamadai ambayo hayajalipwa.
Alisema kuwa kabla ya kulipa madeni hayo lazima yafanyiwe uhakiki ili kujua
uhalali wake. Aidha, aliwataka walimu kufuata taratibu na miongozo ya serikali
katika kuwasilisha madai yao na kuhakikisha nyaraka zote halali zinaambatishwa
ili kuondoa usumbufu usio wa lazima.
vilevile, aliwataka walimu kuwa wavumilivu
na kuchapa kazi kwa bidii kwa sababu Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais, Dk.
Magufuli italipa madeni yote halali ya walimu. “Naomba tuunge mkono juhudi za mheshimiwa Rais za kutafuta fedha kwa
ajili ya watanzania. Tumpe muda mheshimiwa Rais, mambo yatakuwa sawa. Mungu
ametupa viongozi wanaotujali” alisema Prof. Ndalichako.
Akiongelea
nidhamu na maadili kwa walimu, Prof. Ndalichako aliwakumbusha walimu kuwa
wanajukumu la kuwalea wanafunzi na kusimamia maadili yao wenyewe na wanafunzi.
“Walimu ni wazazi na walezi, hivyo mnalo jukumu
la kuwalea watoto hawa wa kike ili waweze kufikia malengo yao. Lazima mjivunie
kuacha kumbukumbu nzuri kwa wasichana hawa kwa kuwasaidia kufikia mustakabali
wa maisha yao” alisema Prof. Ndalichako.
Wakati huohuo,
waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia aliahidi wizara yake kutoa kipaombele kwa
mafunzo ya walimu wa lugha za alama ili waweze kujiendeleza kazini.
=30=
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni