Na. Dennis Gondwe, Iringa
Serikali
imeandaa mazingira wezeshi kwa ajili ya vijana kujiajiri katika mkakati wake wa
kukabiliana na tatizo la ajira nchini.
Kauli hiyo
ilitolewa na mkuu wa mkoa wa Iringa, Amina Masenza alipokuwa akiongea na kaimu
Balozi wa Marekani nchini, Inmi Patterson aliyefanya ziara ya kikazi mkoani Iringa
na kumtembelea ofisini kwake jana.
Masenza alisema
kuwa serikali imeandaa mazingira mazuri na wezeshi kwa ajili ya vijana
kujiajiri nchini na mkoa wa Iringa unaendelea kusimamia utekelezaji huo.
Alisema kuwa mazingira hayo ni mkakati wa kuwafanya vijana wafikirie kujiajiri
zaidi kuliko kuajiriwa na serikali kwa sababu serikali haiwezi kuwaajiri vijana
wote nchini.
“Muitikio wa vijana kujiajiri
ni mkubwa, mfano katika sekta ya kilimo vijana wengi wamejiajiri na kupata
matokeo mazuri katika mavuno hivyo kukuza kipato chao na wengine kuajiri wenzao
kupitia kilimo” alisema Masenza.
Kaimu Balozi wa Marekani
nchini Tanzania, Inmi Patterson alipongeza juhudi hizo za serikali na uongozi
wa mkoa wa Iringa katika kutengeneza mazingira mazuri ya ajira kwa vijana. “Kwa mipango hiyo, kuna mustakabali mzuri kwa
vijana” alisema Patterson.
Aidha, alisisitiza kuwa elimu kwa vijana ni
muhimu katika kufikia maendeleo ya kiuchumi na kijamii. “Vijana bila elimu
hakuna maendeleo” alisema Patterson.
Akiongelea
utawala bora katika sekta ya afya, Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Wamoja Ayubu
alisema kuwa mkoa wa Iringa umepiga hatua katika dhana ya utawala bora na uwazi
katika sekta ya afya. “Mkoa wa Iringa
umeendelea kuimarisha uwazi katika utoaji huduma ili kuondoa mianya ya rushwa.
Huduma zinazotolewa katika hospitali zetu pamoja na gharama zake zimebandikwa
katika mbao za matangazo ili wananchi waweze kufahamu” alisisitiza Ayubu.
=30=
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni