Na. Dennis Gondwe, Iringa
Marekani
yapongeza jitihada zinazofanywa na Rais Dk John Magufuli za kupambana na
ufisadi nchini.
Pongezi hizo
zilitolewa na kaimu Balozi wa Marekani nchini, Inmi Patterson alipomtembelea Mkuu
wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza ofisini kwake hivi karibuni akiwa katika ziara
ya kikazi. Patterson alisema kuwa ubalozi wake unatambua juhudi zinazofanywa na
Rais Dk Magufuli za kupambana na ufisadi nchini. Aidha, alisema kuwa
amefurahishwa na kauli ya Rais Dk Magufuri ya rushwa haivumiliki kwa namna
yoyote. Aliongelea juhudi zinazofanywa katika maeneo ya kukuza demokrasia,
afya, elimu, uchumi na maendeleo kuwa ni maeneo ya kipaombele.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa,
Amina Masenza alisema kuwa mkoa wake unaendelea na mapambano dhidi ya rushwa
kwa kuwahimiza wananchi kufichua vitendo vyote vya rushwa na viashiria vyake na
pindi watuhumiwa wanapobainika hatua za kisheria zinachukuliwa mara moja.
Aliongeza
kuwa masanduku ya maoni yamewekwa katika maeneo mbalimbali ili kuwawezesha
wananchi kutoa maoni yao juu ya utendaji kazi na malalamiko dhidi ya vitendo
vya rushwa katika kuimarisha utawala bora.
Vilevile, aliongelea mkakati wa
kupandikiza dhana ya kuikataa rushwa kwa vijana wakiwa shuleni, Mkuu wa Mkoa
alisema kuwa klabu za kupinga rushwa zimeanzishwa katika shule za sekondari za
mkoa wa Iringa.
Akiongelea
utawala bora katika sekta ya afya, Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Wamoja Ayubu
alisema kuwa mkoa wa Iringa umepiga hatua katika dhana ya utawala bora na uwazi
katika sekta ya afya.
“Mkoa wa Iringa
umeendelea kuimarisha uwazi katika utoaji huduma ili kuondoa mianya ya rushwa.
Huduma zinazotolewa katika hospitali zetu pamoja na gharama zake zimebandikwa
katika mbao za matangazo ili wananchi waweze kufahamu” alisisitiza Ayubu.
=30=
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni