Na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Changamoto
zinazovikabili vitengo vya ustawi wa jamii katika Halmashauri mkoani Iringa zimekuwa
vikifunika mafanikio yanayopatikana kutokana na utendaji wa maafisa ustawi wa
jamii.
Kauli
hiyo ilitolewa na afisa ustawi wa jamii wa Halmashauri ya wilaya ya Mufindi,
Elisha Nyamara alipokuwa akiwasilisha taarifa ya utendaji kazi wa shughuli za
ustawi wa jamii ngazi ya Halmashauri katika kikao cha uhamasishaji wa shughuli
za ustawi wa jamii kwa kamati ya ulinzi na usalama mkoa wa Iringa na wataalam
wa ofisi ya mkuu wa mkoa jana.
Nyamara
alisema “kitengo cha ustawi wa jamii kimekuwa
na kinakabiliwa na changamoto kadhaa ambazo zinafanya wakati mwingine kuonekana
kuwa majukumu ya maafisa ustawi wa jamii hayatekelezeki ipasavyo lakini ukweli
ni kuwa changamoto huziba mafanikio na kufanya mapungufu katika utendaji
kuonekana zaidi”.
Aliongeza kuwa changamoto hizo zinasababishwa na mifumo,
uelewa, ufinyu wa bajeti na uwezo mdogo wa maafisa ustawi kwa baadhi ya Halmashauri.
Nyamara
alizitaja changamoto hizo kuwa ni uchache wa watumishi. “Uchache wa watumishi ni changamoto kubwa, kwasasa kwenye Halmashauri
zote tano, kuna watumishi 14 tu badala ya watumishi 40 kwenye ngazi ya Halmashauri
huku kukiwa hakuna mtumishi yeyote wa ustawi wa jamii kwenye ngazi ya kata.
Ni maafisa
hao hao wanaopaswa kwenda mahakama ya watoto na ile ya wilaya, kwenda katani na
vijijini kufanya uchunguzi wa kijamii dhidi y ukatili, kwenda dawati la jinsia
na watoto na pia kupokea na kusikiliza migogoro ya ndoa na yote haya ni matakwa
ya kisheria” alisema Nyamara.
Changamoto
nyingine aliitaja kuwa ni kitengo kupewa kiasi kidogo cha fedha katika bajeti
ya mapato ya ndani na kusababisha kushindwa kutekeleza shughuli husika.
“Wakati mwingine hata bajeti unayopewa
inaonekana kwenye kitabu lakini wakati wa kuiomba kutekeleza shughuli husika
unaambiwa hakuna fedha. Jambo hili linachangiwa na mambo mengi ikiwemo watoa
maamuzi kukosa uelewa juu ya ustawi wa jamii, au kwa vile kisiasa mambo haya
hayawajengi zaidi wahusika au wakati mwingine kukosa mtu wa kusemea shughuli
hizi katika vikao vya maamuzi au utendaji” alisema Nyamara.
Changamoto
nyingine ilitajwa na afisa ustawi wa jamii kuwa ni ufinyu wa majengo ya ofisi
za ustawi wa jamii kwenye Halmashauri. “Ofisi
za kitengo cha ustawi wa jamii hufikiriwa katika mtazamo wa watumishi husika
kukaa na kufanya kazi lakini kwamba panahitajika faragha katika utendaji kazi
jambo hilo halipewi kipaumbele. Hata hivyo, hii imefanya kukiuka sheria na
taratibu za kiutendaji kwa vile si haki kuwatendea wateja wetu namna
tunavyowatendea.
Na kwa mazingira hayo wakati mwingine tumeukosa ukweli kutoka
kwa watoto kwani hukosa amani kwa mazingira wanayohojiwa au kutakiwa kutoa
taarifa” alisisitiza Nyamara.
Changamoto
nyingine alizitaja kuwa ni kuongezeka kwa matukio ya ukatili dhidi ya watoto na
watoto wenyewe kujihusisha kwenye matukio makubwa ya ukiukwaji wa sheria za
nchi.
Aliongeza kuwa jamii kushindwa kutoa ushirikiano kwenye masuala ya ulinzi
na usalama wa mtoto kwa kuogopa kuitwa mahakamani. Pia kushindwa kufanikiwa kwa
mashauti ya watoto katika baadhi ya halmashauri.
Ofisi
ya mkuu wa mkoa wa Iringa iliandaa kikao cha uhamasishaji shughuli za ustawi wa
jamii kwa kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa, wataalam ofisi hiyo na Halmashauri
ili kuwajengea uelewa wa masuala ya ulinzi wa mtoto.
=30=
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni