Na
Mwandishi Maalum, IRINGA
Watumishi wa umma mkoani Iringa wametakiwa
kufanya kazi kwa weledi na nidhamu katika kutekeleza majukumu yao
wanapowahudumia wananchi.
Kauli hiyo ilitolewa na Katibu Tawala mkoa
wa Iringa, Wamoja Ayubu alipokuwa akifungua mafunzo elekezi ya awali kwa
watumishi wapya wa umma walioajiliwa katika ofisi ya mkuu wa mkoa wa Iringa, mafunzo
yalifanyika katika ukumbi wa hospitali ya rufaa ya mkoa wa Iringa jana.
Ayubu alisema kuwa msingi wa utumishi wa
umma umejikita katika uadilifu, hivyo mtumishi wa umma lazima afanye kazi kwa
weledi na nidhamu ya hali ya juu. Aliongeza kuwa serikali ya awamu ya tano
chini ya Rais Dr John Magufuli imejipambanua kwa kusimamia nidhamu na
uwajibikaji kwa watumishi wa umma.
Aliwataka watumishi wa umma mkoani Iringa
kuwa mfano mzuri wa kuingwa katika nidhamu na uwajibikaji wanapowahudumia
wananchi ili wabaki na kumbukumbu ya huduma njema.
Akiongelea umuhimu wa mafunzo elekezi ya
awali kwa watumishi wa umma, Katibu Tawala mkoa alisema kuwa watumishi wengi
wanatoka katika maeneo tofauti yenye mitazamo tofauti hivyo, kuitaji
kufundishwa utaratibu wa kazi katika serikali.
“Mafunzo haya ni muhimu sana unapoingia katika utumishi wa umma.
Tunatoka katika vyuo tofauti na tamaduni tofauti hivyo, hata tabia zinakuwa
tofauti. Mafunzo haya yanalenga kutufundisha namna utumishi wa umma ulivyo na
jinsi mtumishi wa umma anavyotakiwa kuonekana na kutenda kazi” alisema
Ayubu.
Aliwataka watumishi hao kubadilika baada ya
mafunzo kimtazamo na kiutendaji na kuzingatia viwango vya juu katika utumishi
wao.
“Unajua unapoingia katika utumishi
wa umma, unajikuta unafanya makosa, ila tunashindwa kukuchukulia hatua za
kiutumishi badala yake tunalazimika kukufanyia ushauri
zaidi. Tunabadilika na kuwa wazazi na walezi katika kuwaelimisha
watumishi” alisema Ayubu.
Aliongeza kuwa baada ya mafunzo haya watakuwa
wakiwachukulia hatua stahili za kiutumishi watumishi wote watakaotenda kinyume
na maadili ya utumishi wa umma.
Alisema kuwa katika mafunzo hayo watumishi
wa umma watafundishwa muundo wa serikali, uendeshaji wa shughuli za serikali,
utunzaji wa kumbukumbu, maadili ya utumishi wa umma, maboresho ya utumishi wa
umma, huduma kwa mteja, sheria ya utumishi wa umma namba 8 ya mwaka 2002 na
kanuni zake, mpango wa kudhibiti ukimwi kwa watumishi wa umma na upimaji wa
wazi utendaji kazi kwa watumishi wa umma.
Mafunzo elekezi ya awali ya siku tano kwa
watumishi wapya wa umma yameandaliwa na ofisi ya mkuu wa mkoa wa Iringa kwa
kushirikiana na chuo cha utumishi wa umma (TPSC) yakishirikisha watumishi wapya
107 kutoka ofisi ya mkuu wa mkoa, ofisi za wakuu wa wilaya ya hospitli ya rufaa
ya mkoa.
=30=
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni