Jumapili, 12 Novemba 2017

MAELEZO MAFUPI YA KATIBU TAWALA MKOA WA IRINGA BIBI WAMOJA AYUBU WAKATI WA UZINDUZI WA KAMPENI YA MAMA MSOSI LISHE KIMKOA KATIKA MANISPAA YA IRINGA, TAREHE 11 NOVEMBA, 2017



MAELEZO MAFUPI YA KATIBU TAWALA MKOA WA IRINGA BIBI WAMOJA AYUBU WAKATI WA UZINDUZI WA KAMPENI YA MAMA MSOSI LISHE KIMKOA KATIKA MANISPAA YA IRINGA, TAREHE 11 NOVEMBA, 2017

Mheshimimiwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa,
Waheshimiwa Wakuu wa Wilaya,
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Iringa,
Waheshimiwa Madiwani,
Waheshimiwa Viongozi wa Vyama vya Siasa,
Ndugu Viongozi wa Madhehebu ya Dini,
Watendaji Wote kutoka Serikalini,
Wawakilishi wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali,
Waandishi wahabari
Wageni Waalikwa wote,
Mabibi na Mabwana. 

Awali ya yote napenda nichukue fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu, kwa kutuwezesha kukutana salama siku ya leo ambayo Kimkoa tunazidua kampeni ya Mama Msosi Lishe ikiwa na lengo la kupambana na tatizo la utapiamlo Hususani  udumavu Mkoani Iringa. 

Kipekee napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwako Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa kwa kukubali kwako mwaliko wa kuwa Mgeni Rasmi katika uzinduzi wa kampeni hii muhimu. Napenda nitumie fursa hii kuushukuru uongozi wa Manispaa ya Iringa kwa kukubali kuwa wenyeji wa uzinduzi huu na kuhakikisha kuwa unafanikiwa.

Vilevile, niwashukuru  wananchi wote mliopo hapa kwa kutenga muda wenu na kuja kushiriki kampeni hii. Kuwepo kwenu hapa ni ushahidi  tosha unaoonyesha mnavyojali na kuchukulia uzito masuala yanayohusu mapambano dhidi ya  udumavu ambao umeendelea kuwa tatizo katika Mkoa wetu.

Mheshimiwa Mgeni Rasmi,
Chimbuko la uzinduzi ya kampeni ya kupambana na utapiamlo hususani udumavu linatokana na Mkoa wetu kuwemo miongoni mwa Mikoa 5 ya Tanzania yenye kiwango kikubwa   cha udumavu, kwa mujibu wa utafiti wa viashiria vya afya (TDHS, 2015/2016) Mkoa wetu umefikia asilimia 42 ya udumavu.

Mheshimiwa Mgeni Rasmi,
Changamoto kubwa katika Mkoa wa Iringa ni uelewa mdogo katika jamii wa masuala ya Lishe, mfano;

  • Uandaaji wa chakula hasa ugali kwa kutumia mahindi yaliolowekwa kwa muda mrefu  maarufu kama ‘kiverege’ hupelekea madini na vitamini zote kupotea,

  • Watoto wadogo kulishwa milo ya watu wazima isiyozingatia vyakula mchanganyiko, idadi ya milo na kiasi cha chakula cha kumpa mtoto kulingana na umri hasa kipindi mtoto anapotimiza  miezi 6 mpaka miaka miwili.

  • Ushiriki mdogo wa akinababa katika ufuatiliaji wa makuzi na maendeleo ya mtoto hivyo kumwachia mama majukumu yote.
  • Kuchelewa kuanza kliniki ya uzazi ili kupata huduma za muhimu kama vidonge vya kuongeza damu, kusaidia ukuaji bora wa mtoto, dawa za minyoo na kuzuia Malaria na VVU/UKIMWI kwa akinamama wajawazito


Kutokana na hali hiyo, Ofisi ya Mkoa wa Iringa kwa kushirikiana na wadau imeandaa shindano la mama msosi lishe  ambalo litakalohusisha wanawake watakao andaa chakula bora cha familia na kupimwa uelewa wao juu ya umuhimu wa lishe bora, usafi wa mazingira yanayomzunguka na matumizi ya nishati mbadala ili kupunguza uharibifu wa mazingira.

Pia napenda kueleza kuwa katika kipindi hiki cha kampeni  washindi 54 waliofanya vizuri kutoka  kata  zote  18 watapewa tuzo ya ushindi, baada ya hapo washindi 54 watashindanishwa na kupata washindi 3 bora ngazi ya Halmashauri watakaopewa tuzo ya ushindi ya Halmashauri,  tunaamini kwa kufanya hivyo washindi hawa wataweza kuwa kichocheo cha mabadiliko katika Mkoa wetu. 

Aidha zoezi hili la kampeni zitaendelea katika Halmashauri zingine za Mkoa wa Iringa.  

Aidha, Serikali kwa kushirikiana na wadau  mbalimbali wa maendeleo wakiwemo, wanasiasa, viongozi wa dini, mashirika ya hiyari tumeamua  kutumia kampeni hii kuhamasisha na kuelimisha jamii ili kupunguza kabisa tatizo la udumavu. 

Vilevile, Kampeni hii itatuwezesha kutafakari mafanikio na changamoto ambazo tumekuwa tukikabiliana nazo kwa lengo la kuandaa mipango na mikakati itakayosaidia kupunguza tatizo hili katika familia kwa watoto chini ya miaka 5 na wanawake walio katika umri wa uzazi.

Mheshimiwa Mgeni Rasmi,
Kaulimbiu ya Mwaka 2017 ya kukabiliana na udumavu katika Mkoa ni ‘’Mama Msosi lishe”

Kaulimbiu hii  inaendena na muktadha na vipaumbele vya Mkoa kwa sasa kwa kuzingatia kwamba mazingira rafiki ya kutolea elimu kwa jamii imekuwa ni  changamoto  hususani wanajamii kutojitokeza pindi elimu itolewapo na wadau. Kwa kuzingatia  Kaulimbiu hii sote kwa pamoja tushirikiane  kutafuta suluhisho la kudumu la changamoto ya udumavu  ambayo ni kubwa katika jamii yetu. 

Sambamba na changamoto ya udumavu suala la kutokuzingatia kanuni za usafi wa mazingira na matumizi hafifu ya nishati mbadala bado limeendelea kuwa changamoto kwa jamii.

Kutokana na changamoto hizi Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali za kukabiliana na tatizo la udumavu, uhalibifu  wa mazingira, uchafuzi wa mazingira kwa kutoa elimu kwa jamii ili kukabiliana na changamoto hizo. Serikali kwa kushirikiana na wadau tunaahidi kwamba tutaendelea kutoa elimu kwa jamii juu ya afua mbalimbali za Lishe, afya na usafi wa mazingira na matumizi ya nishati mbadala.

Mheshimiwa Mgeni Rasmi,
Shukrani
Nitumie fursa hii pia kuwashukuru wote waliojitolea kwa hali na mali kuhakikisha kuwa uzinduzi wa kampeni hii unafanikiwa. wakiwemo mashirika  yote ya hiari hapa mkoani (CUAMM, Mwanzo bora, NAFAKA, WARIDI, TAHEA MIHAN GAS N.K.) kwa misaada yao ya hali na mali iliyoifanya kampeni hii ifanikiwe. 

Kipekee niwashukuru, Vyombo vya Habari kwa ushirikano waliouonyesha.

ASANTENI SANA KWA KUNISIKILIZA

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Habari zinazoendelea hivi sasa

SERIKALI KUWEZESHA VIJANA KUKOPA

Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Iringa Serikali itaendelea kuwawezesha vijana kwa kuwatengenezea mazingira mazuri ya mikopo ili waweze k...