Jumapili, 12 Novemba 2017

HOTUBA YA MKUU WA MKOA WA IRINGA MHESHIMIWA AMINA MASENZA KATIKA UZINDUZI WA KAMPENI YA MAMA MSOSI LISHE ILIYOFANYIKA KATIKA BUSTANI YA MANISPAA YA IRINGA TAREHE 11 NOVEMBA, 2017




HOTUBA YA MKUU WA MKOA WA IRINGA MHESHIMIWA AMINA MASENZA KATIKA UZINDUZI WA KAMPENI YA MAMA MSOSI LISHE ILIYOFANYIKA KATIKA BUSTANI YA MANISPAA YA IRINGA TAREHE 11 NOVEMBA, 2017




Ndugu Katibu Tawala Mkoa,
Waheshimiwa Wakuu wa Wilaya,
Ndugu, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Iringa,
Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa,
Ndugu Viongozi wa Dini,
Ndugu Viongozi wa Kisiasa,
Wadau wote wa Masuala ya Lishe Mkoa wa Iringa,
Waandishi wa Habari,
Mabibi na Mabwana


Awali ya yote napenda nichukue fursa hii kuwakaribisha katika uzinduzi wa Kampeni ya MAMA MSOSI LISHE katika Mkoa wa Iringa. Kwa niaba ya Mkoa wa Iringa napenda kuwashukuru viongozi na wadau wote walioshiriki kwa hali na mali katika maandalizi na hatimae kuwezesha uzinduzi wa kampeni hii.

Lengo la Kampeni ya Mama Msosi Lishe ni kutoa hamasa kwa jamii kuhusu Lishe Bora kwa familia, Usafi wa Mazingira na matumizi ya Nishati mbadala ili kuboresha rasilimali ya Misitu.

Ndugu Wananchi,
Kampeni ya Mama Msosi Lishe ni mojawapo ya njia ya kuboresha Lishe kwa familia na kuondoa matatizo yanayosababishwa na Lishe duni. Wataalam wa masuala ya Lishe wanatuambia kuwa watoto waliopata huduma bora za Lishe, katika kipindi cha siku 1,000 za kwanza za uhai wao ambazo zinaanza tangu mama anapopata ujauzito hadi mtoto anapotimiza umri wa miaka miwili wanapata faida zitakazodumu katika maisha yao yote.

Hiki ndicho kipindi mtoto anapojenga msingi wa ukuaji wa mwili na maendeleo ya akili. Kwa bahati mbaya madhara ayapatayo mtoto katika ukuaji wake kimwili na maendeleo ya kiakili kutokana na Lishe duni katika siku 1,000 za kwanza za maisha yake hayawezi kurekebishwa kwa maisha yake yote.

Faida hizo ni:-
·        Maendeleo mazuri ya ukuaji wa ubongo,
·        Uwezo mzuri wa kukabiliana na maradhi,
·        Uwezo mzuri wa kiakili,
·        Uwezo na ufanisi wa kujifunza,
·        Uwezo mkubwa wa kujiingizia kipato wakiwa watu wazima.


Ndugu Wananchi,
Suala la Lishe ni mtambuka. Hivyo, katika jamii utapiamlo ni matokeo ya mkusanyiko wa matatizo mengi yanayotokana na mpangilio usio mzuri wa chakula na ulaji mbaya wa chakula. Matatizo hayo ni:


  • Ulaji duni usiokidhi viwango vya virutubishi vyote vinavyotakiwa katika mwili, 
  • Maradhi mbalimbali,
  • Kutokuwa na uhakika wa chakula,
  • Matunzo duni ya wanawake na watoto,
  • Mazingira machafu na huduma duni za Afya,
  • Rasilimali haba na mgawanyo usiokuwa na uwiano sahihi,
  • Umaskini wa kipato,



Ndugu Wananchi,
Sote tunapaswa kufahamu kwamba Lishe duni kwa wanawake wajawazito inawaweka katika mazingira yanayoweza kusababisha kujifungua watoto njiti, waliokufa, kuharibika kwa mimba, kuzaa watoto wenye vichwa vikubwa, kuzaa watoto wenye mgongo wazi, kuwadhoofisha wanawake wajawazito na hivyo kuugua mara kwa mara, kupoteza maisha wakati au baada ya kujifungua. Vifo vya wanawake wajawazito vitapungua sana endapo watakuwa na hali nzuri ya Lishe katika kipindi chote cha ujauzito. 

Pia tunafahamu kuwa athari nyingine za Lishe duni kwa mwanadamu ni pamoja na tezi la shingo (Goita), upofu, kudhoofisha kinga ya mwili, kupata vidonda kinywani na fizi kutoka damu. 

Kwa mujibu wa utafiti (TDHS, 2015/2016) umebaini kuwa hali ya Lishe ya wanawake na watoto bado ni mbaya Mkoani Iringa. Asilimia 28 ya wanawake wajawazito wana upungufu wa damu. Asilimia 42 ya watoto wamedumaa, asilimia 13.8 wana uzito pungufu, asilimia 3.6 wana ukondefu na asilimia 7.2 tu ndiyo wanalishwa vyakula vya nyongeza ipasavyo.

Ndugu Wananchi,
Mkoa wa Iringa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali umekuwa ukichukua hatua za kukabiliana na tatizo la utapiamlo. Hatua hizo ni pamoja na kutoa elimu ya Lishe katika vituo vya kutolea huduma, kutoa matibabu ya utapiamlo, kuhamasisha jamii kubadilli tabia za ulaji usiofaa na kufuata mtindo bora wa maisha, kuhamasisha usafi wa mazingira, kuwahi kliniki pindi mama anapogundua kuwa mjamzito.

Ndug Wananchi,
Serikali ya Awamu ya Tano inatambua umuhimu wa kuwekeza katika masuala ya Lishe kama mkakati mmojawapo wa kufanikisha azma ya Serikali kufikia uchumi wa kipato cha kati na viwanda ifikapo 2025. Baraza la Umoja wa Mataifa liliweka azimio la kuwa kati ya mwaka 2016 hadi mwaka 2025 ni miaka ya "Kuchukua Hatua katika Kutekeleza Masuala ya Lishe - Decade of Action on Nutrition". 

Hivyo, wito wangu kwa wananchi wa Mkoa wa Iringa, tuunge mkono juhudi zinazofanywa na Serikali yetu katika kupambana na tatizo la utapiamlo. Tukishirikiana pamoja katika kuunga mkono juhudi hizi kutatuwezesha kufikia adhima ya kuwa nchi ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

Ndugu Wananchi,
Katika kukabiliana na tatizo la utapiamlo ni vizuri elimu bora itolewe kwa jamii juu ya:

  • Uandaaji wa chakula kwa sababu maeneo mengi huloweka mahindi muda mrefu na kupoteza madini na vitamini

  •  Ulishaji wa watoto wadogo uzingatie vyakula mchanganyiko, idadi ya milo na kiasi cha chakula cha kumpa mtoto kulingana na umri kuanzia kipindi mtoto anapotimiza miezi 6 mpaka miaka miwili.

  • Kina baba washiriki kikamilifu katika ufuatiliaji wa makuzi na maendeleo ya mtoto pasipo kumuachia mama pekee.
  • Kina mama wajawazito lazima waanze mapema kliniki ya uzazi ili kupata huduma muhimu kama vidonge vya kuongeza damu, kusaidia ukuaji bora wa mtoto, dawa za minyoo, kuzuia Malaria na VVU. Katika jambo hili, niombe ushiriki wa kina baba katika kuwaruhusu na kuwasindikiza kliniki kina mama.



Ndugu Wananchi,
Kabla sijamaliza hotuba yangu, nitoe rai kwenu kuwa Kampeni ya Mama Msosi Lishe ilete mabadiliko chanya katika jamii nzima. Tufuatilie kwa makini mada zitakazowasilishwa kupitia vyombo vya habari na vipindi vya mjadiliano, wahudumu wa ngazi ya jamii, wadau na wataalamu mbalimbali katika vituo vya kutolea huduma za afya ili kupata elimu na ufahamu zaidi kuhusu masuala ya Lishe.

Ni wajibu wa kila mmoja wetu, kwa nafasi yake kujitolea kwa dhati kuleta hali bora ya Lishe kwake, kwa familia yake na kwa Wanairinga wote.

Ndugu wananchi, baada ya kusema hayo,

“NATAMKA RASMI KUWA KAMPENI YA MAMA MSOSI LISHE IMEZINDULIWA”

Asanteni kwa kunisikiliza!




Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Habari zinazoendelea hivi sasa

SERIKALI KUWEZESHA VIJANA KUKOPA

Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Iringa Serikali itaendelea kuwawezesha vijana kwa kuwatengenezea mazingira mazuri ya mikopo ili waweze k...