Jumapili, 12 Novemba 2017

WABABA IRINGA WATAKIWA KUSHIRIKI MAKUZI NA MAENDELEO YA WATOTO



Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Iringa

Wakina baba mkoani Iringa watakiwa kushiriki kikamilifu katika makuzi na maendeleo ya watoto ili kujenga jamii familia imara isiyokuwa na utapiamlo.

Kauli hiyo ilitolewa na mkuu wa mkoa wa Iringa, Mheshimiwa Amina Masenza akipokuwa akizindua kampeni ya Mama Msosi Lishe katika bustani ya Manispaa ya Iringa jana.

Mheshimiwa Masenza alisema kuwa Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dr John Magufuli inatambua umuhimu na kuwekeza katika masuala ya lishe nchini. 
 
Mkuu wa Mkoa wa Iringa Mhe Amina Masenza (kulia) akizindua kampeni ya Mama Msosi Lishe kwa kumnywesha uji mtoto Pricila Mgaya
Huo ni mojawapo ya mkakati wa kufanikisha azma ya Serikali kufikia uchumi wa kipato cha kati na viwanda ifikapo 2025. Baraza la Umoja wa Mataifa liliweka azimio la kuwa kati ya mwaka 2016 hadi mwaka 2025 ni miaka ya kuchukua Hatua katika kutekeleza masuala ya lishe” alisema mheshimiwa Masenza. 
Aliwataka wananchi wa mkoa wa Iringa kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Serikali katika kupambana na tatizo la utapiamlo.

Aidha, aliwataka kina baba kushiriki kikamilifu katika ufuatiliaji wa makuzi na maendeleo ya watoto pasipo kuwaachia kina mama peke yao. Alisema kuwa hiyo ni njia ya kukabiliana na tatizo la utapiamlo mkoani Iringa. Njia nyingine aliitaja kuwa ni uandaaji wa chakula vizuri kutokana na maeneo mengi huloweka mahindi muda mrefu na kupoteza madini na vitamin. 

Aliongeza kuwa ulishaji wa watoto wadogo uzingatie vyakula mchanganyiko, idadi ya milo na kiasi cha chakula cha kumpa mtoto kulingana na umri kuanzia kipindi mtoto anapotimiza miezi 6 mpaka miaka miwili. 

Vilevile, aliwataka kina mama wajawazito kuanza mapema kliniki ya uzazi ili kupata huduma muhimu. Alizitaja huduma hizo muhimu kuwa ni kupata vidonge vya kuongeza damu, kusaidia ukuaji bora wa mtoto, dawa za minyoo, kuzuia Malaria na VVU.

Katika maelezo ya awali ya Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, yaliyotolewa na Katibu Tawala msaidizi, Sehemu ya Mipango na Uratibu, Nuhu Mwasumilwe alisema kuwa changamoto kubwa katika Mkoa wa Iringa ni uelewa mdogo katika jamii wa masuala ya lishe. Changamoto hizo alizitaja kuwa ani uandaaji wa chakula hasa ugali kwa kutumia mahindi yaliolowekwa kwa muda mrefu  maarufu kama ‘kiverege’ husababisha madini na vitamini zote kupotea. 

Changamoto nyingine ni watoto wadogo kulishwa milo ya watu wazima isiyozingatia vyakula mchanganyiko na ushiriki mdogo wa akinababa katika ufuatiliaji wa makuzi na maendeleo ya mtoto hivyo kumwachia mama majukumu yote. Na wakina mama wajawazito kuanza kliniki ya uzazi kwa kuchelewa.

Alisema kuwa changamoto hizo ziliifanya Ofisi ya Mkoa wa Iringa kwa kushirikiana na wadau kuandaa shindano la Mama Msosi Lishe litakalohusisha wanawake watakao andaa chakula bora cha familia. Aliongeza kuwa katika uandaaji huo, watapimwa uelewa wao juu ya umuhimu wa lishe bora, usafi wa mazingira yanayomzunguka na matumizi ya nishati mbadala ili kupunguza uharibifu wa mazingira.

Kampeni ya Mama Msosi Lishe mwaka 2017 inaongozwa na kaulimbiu isemayo ‘Mama Msosi lishe’. Chimbuko lake ni kupambana na utapiamlo hasa udumavu kutokana na Mkoa wa Iringa kuwa miongoni mwa Mikoa 5 ya Tanzania yenye kiwango kikubwa cha udumavu, kwa mujibu wa utafiti wa viashiria vya afya (TDHS, 2015/2016) ukiwa na asilimia 42 ya udumavu.
=30=

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Habari zinazoendelea hivi sasa

SERIKALI KUWEZESHA VIJANA KUKOPA

Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Iringa Serikali itaendelea kuwawezesha vijana kwa kuwatengenezea mazingira mazuri ya mikopo ili waweze k...