Jumapili, 28 Januari 2018

CCM MUFINDI YARIDHISHWA NA KAZI ZA SERIKALI



Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Iringa
Chama cha mapinduzi wilayani Mufindi kinaridhishwa na kazi zinazofanywa na serikali ya awamu ya tano katika utekelezaji wa ilani yake na kuwahudumia wananchi.

Kauli hiyo ilitolewa na mwenyekiti wa chama cha mapinduzi Wilaya ya Mufindi, Daud Yassin katika ziara ya mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza alipotembelea shule ya msingi Igombavanu kukagua miundombinu ya shule hiyo na kuongea na wanufaika wa mpango wa kunusuru kaya masikini TASAF wilayani humo.

Yassin alisema “CCM wilayani Mufindi tunafarijika na kazi zinazofanywa na serikali ya awamu ya tano chini ya uongozi wa Rais Dr. John Magufuli na wasaidizi wake. Aidha, tunaridhika na ushirikiano tunaoupata kutoka kwa mkuu wa Mkoa wa Iringa na mkuu wa Wilaya ya Mufindi katika kusimamia utekelezaji wa Ilani yetu”. 

Alisema kuwa kazi ya chama cha mapinduzi ni kuisimamia serikali ili itekeleze Ilani na maendeleo kwa wananchi. Aliongeza kuwa lengo la kuisimamia serikali kutekeleza Ilani ni kuhakikisha maisha ya wananchi wilayani Mufindi yanabadilika na kuwa bora zaidi.

Mwenyekiti huyo aliipongeza serikali kwa uanzishaji wa mpango wa kunusuru kaya masikini nchini. Alisema kuwa mpango huo umesaidia kurudisha matumaini kwa wananchi wasio na uwezo na kuwawezesha kujikimu kimaisha. “Hizi ni juhudi za makusudi zinazofanywa na serikali kuonesha jinsi inavyojali maisha ya wananchi wake” alisema.

Akiongea na wamufaika wa mpango wa kunusuru kaya masikini katika kijiji cha Igombavanu mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza alisema kuwa serikali inawajali wananchi wake na kutaka wawe na uhakika wa kula milo mitatu kwa siku. 

Mfuko wa TASAF umewakomboa wananchi wengi kutoka katika maisha duni. Na huu ndiyo upendo thabiti wa serikali kwa wananchi wake” alisema Masenza. Kupitia TASAF familia zimenufaika na watoto wanaohudhuria shule wamenufaika kwa elimu na afya aliongeza.

Mfuko wa maendeleo ya jamii TASAF unatekeleza mpango wa kunusuru kaya masikini katika Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi kwa vijiji 75 vikiwa na wanufaika 6,279.
=30=

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Habari zinazoendelea hivi sasa

SERIKALI KUWEZESHA VIJANA KUKOPA

Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Iringa Serikali itaendelea kuwawezesha vijana kwa kuwatengenezea mazingira mazuri ya mikopo ili waweze k...