Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Mkuu
wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza ameiagiza Halmashauri ya Mji wa Mafinga
kuwafidia wanufaika wote wa mpango wa kunusuru kaya masikini ambao kuku wao
wamekufa kutokana na ugonjwa wa kideri.
Agizo
hilo alilitoa katika shule ya msingi ya Mafinga alipofanya ziara ya
kuwatembelea wanufaika wa TASAF na kukagua shughuli wanazofanya katika mji wa Mafinga.
Masenza
alisema kuwa amepokea kwa masikitiko taarifa zilizotolewa na wanufaika wa
mpango wa kunusuru kaya masikini ambao walijinyima na kuanzisha ufugaji wa kuku
kwa lengo la kujikwamua, lakini kuku wao wamekufa.
“Naitaka Halmashauri ya mji wa Mafinga kuwafidia kuku wote waliokufa
kutokana na kideri na sababu nyingine kwa sababu wataalam wa Halmashauri
kushindwa kuwatembelea na kuwashauri vizuri juu ya ufugaji wa kuku”
aliagiza Masenza.
Aidha,
alitumia kikao hicho kuwaagiza wataalam wa Halmashauri kuwatambua kwa majina,
sehemu wanazokaa na shughuli wanazofanya wanufaika wa mpango wa TASAF.
“Watendaji tokeni ofisini na kuwafuata
wananchi walipo ili muweze kushauri na kutatua matatizo yao. Lazima mtambue
kuwa mpo katika nafasi hizo kwa ajili ya kuwahudumia wananchi. kukaa ofisini
wakati wananchi wanashindwa kutatua matatizo yao hamuwatendei haki. Mtaalam
yeyote atakayekaidi maelekezo haya anatafuta ugomvi na mimi” alisema Masenza.
Leticia
Sanga ambaye ni mnufaika wa TASAF aliamua kubadilisha mtazamo wa kufuga kuku na
kujenga nyumba ya kawaida baada ya kuona kuku alionunua kwa fedha ya TASAF
wakifa mfululizo.
“Mimi niliona
nijiongeze sababu nilikuwa nafuga kuku lakini kuku wakawa wanakufa hadi kufikia
kuku 10. Nikaona nikiulizwa fedha za TASAF nimefanyia nini nitakosa majibu
nikaamua kujiongeza kujenga nyumba” alisema Sanga.
=30=
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni