Na. Ofisi
ya Mkuu wa Mkoa
Mkoa wa Iringa umefanikiwa kuongeza pato lake hadi
kufikia zaidi ya shilingi trilioni tano mwaka 2016 na kuufanya kuwa Mkoa wa
tano kwa kigezo cha GDP kitaifa.
Kauli hiyo ilitolewa na mkuu wa Mkoa wa Iringa,
Amina Masenza alipokuwa akiwasilisha taarifa fupi ya Mkoa wa Iringa kwa wajumbe
kutoka Chuo cha Taifa cha Ulinzi Tanzania waliofanya ziara ya mafunzo ya siku
tano mkoani Iringa katika ukumbi wa ofisi ya mkuu wa Mkoa.
Masenza alisema “pato la Mkoa wa Iringa (GDP) limeongezeka kutoka shilingi
trilioni 2.3 mwaka 2010 hadi kufikia shilingi trilioni 5.10 Mwaka 2016, wakati pato la mkazi [Per Capita GDP) mwaka
2010 lilikuwa shilingi 1,330,118 ambalo limeongezeka hadi kufikia shilingi 2,982,569 mwaka 2016”. Aliongeza kuwa takwimu hizo
za (GDP) kwa
mwaka 2016, Mkoa wa Iringa umekuwa ni Mkoa wa tano kwa ngazi ya GDP kitaifa na
Mkoa wa tatu kwa pato la mkazi ukitanguliwa na Mkoa wa Dar es Salaam na Mbeya.
Aliongeza kuwa pato la Mkoa huchangiwa kwa kiasi kikubwa na mashamba
makubwa ya chai, viwanda vya chai, misitu, viwanda vya mbao na tumbaku.
Akiongelea shughuli za
kiuchumi, mkuu wa Mkoa alizitaja kuwa ni kilimo, ufugaji, upasuaji mbao,
uvuvi, biashara, ajira za ofisini na viwandani. “Asilimia 75 ya wakazi wa Mkoa huu hujishughulisha zaidi na Kilimo
pamoja na ufugaji. Mazao ya kilimo yanayolimwa katika Mkoa huu ni mahindi,
maharage, mpunga, ngano, viazi, pareto, chai, matunda, alizeti, karanga, ufuta,
nyanya, vitunguu, tumbaku, soya na mtama” alisema Masenza.
Nae kiongozi wa msafara wa wajumbe
kutoka Chuo cha Ulinzi cha Taifa, Kapten Msafiri Hamisi alipongeza juhudi
zinazofanywa na serikali ya Mkoa katika kuwahudumia wananchi. Aidha, alishukuru
mapokezi waliyopewa na uongozi wa Mkoa na kuomba ushirikiano huo uwe undelevu.
Akitoa neno la shukrani, kiongozi wa wajumbe kutoka
chuo cha Taifa cha ulinzi Capt. Msafiri Hamisi alipongeza kwa mapokezi ya Mkoa
na kazi zinazofanywa na Mkoa za kuwahudumia wananchi na kuwaletea maendeleo.
Aidha, aliahidi wanafunzi wa chuo cha Taifa cha ulinzi kuwa balozi wazuri kwa
mkoa wa Iringa.
Kwa
matokeo ya Sensa ya mwaka 2012 Mkoa wa Iringa ulikuwa na watu 941,238 kati ya
hao wanaume walikuwa 452,052 na wanawake 489,186 na wastani wa ongezeko la
idadi ya watu kwa mwaka ni asilimia 1.1. Makadirio ya idadi ya watu kwa mwaka
2017 ni watu 1,000,040; wanaume wakiwa 480,293 na wanawake 519,747.
=30=
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni