Jumanne, 11 Februari 2014

DKT. ISHENGOMA : UFANYENI MTAMA ZAO LA CHAKULA



Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa

Wakulima wa halmashauri ya wilaya ya Iringa wametakiwa kulima zao la mtama na kulifanya zao la chakula ili kukabiliana na upungufu wa chakula unaoikabili halmashauri hiyo kutokana na hali ya ukame wa mara kwa mara.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma (katikati)
Kauli hiyo imetolewa na mkuu wa mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma alipokuwa akiongea na viongozi na wananchi wa kata za Itunundu na Pawaga katika shule ya sekondari William Lukuvi iliyopo katika halmashauri ya wilaya ya Iringa.

Mkuu wa mkoa wa Iringa amesema kuwa kutokana na ukame wa mara kwa mara unaosababishwa na mabadiliko ya tabia nchi, umefika wakati kwa wananchi wa kata za Itunundu na Pawaga kulima zao la mtama. Amesema kuwa suala si kulima tu zao la mtama, bali pia kulifanya zao hilo kuwa zao la chakula. Amesema kufanya hivyo kutawawezesha wananchi kuwa na uhakika wa chakula kwa mwaka mzima na kuepuka tatizo la njaa.

Mkuu wa mkoa wa Iringa amewataka wananchi mkoani Iringa kuhakikisha wanapanda miti ya kutosha ili kukabiliana na changamoto ya mabadiliko ya tabia nchi yanayosababisha ukame katika baadhi ya maeneo ya mkoa wa Iringa. 

Amesema kuwa upandaji miti huo uende sambamba na upandaji wa miti ya matunda. Aidha, ameshauri kuwa ni vema taasisi mbalimbali zikajikita katika upandaji wa miti ya matunda kama mapapai, maembe na maparachichi.  

Katika kuonesha umuhimu wa upandaji miti, mkuu wa mkoa wa Iringa alishiri katika upandaji wa mti pamoja na viongozi alioambata nao katika ziara hiyo.

Mkuu wa Mkoa wa Iringa akipanda mti
=30=


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Habari zinazoendelea hivi sasa

SERIKALI KUWEZESHA VIJANA KUKOPA

Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Iringa Serikali itaendelea kuwawezesha vijana kwa kuwatengenezea mazingira mazuri ya mikopo ili waweze k...