Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Serikali imezipongeza shule zisizo za serikali kwa kufanya
vizuri katika matokeo ya kitaifa kwa mitihani ya kuhitimu darasa la saba,
kidato cha nne na sita kanda ya Nyasa.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt.
Christine Ishengoma katika hotuba yake iliyosomwa kwa niaba yake na Mkuu wa
Wilaya ya Kilolo, Gerald Guninita katika ukumbi wa mikutano wa hoteli ya
Kalenga mjini Iringa.
Dkt. Ishengoma amesema “niwapongeze sana kwa namna ya pekee
kutokana na ukweli kwamba, ninyi mmekuwa ni mfano bora wa malezi ya mtoto wa
kike kwani mara nyingi wanafunzi hufanya vizuri kitaifa katika matokeo ya
mitihani ya kuhitimu darasa la saba, kidato cha nne na cha sita. Shule zisizo
za serikali zinaongoza katika kufanya vizuri”.
Amesema kwa matokeo haya
inaonesha wazi mmejipanga vizuri kulisaidia taifa kutoa elimu yenye manufaa na
tija kwa watanzania.
Amesema mafanikio hayo yanadhihirisha nia njema waliyonayo
wamiliki wa shule binafsi katika kulielimisha na kuliendeleza taifa. Amepongeza
juhudi za kukutana na kujadili na kupeana uzoefu na kubadilishana mbinu za
ufundishaji katika kutoa elimu bora kwa wanafunzi.
Mkuu wa Mkoa amesema kuwa pamoja na kufanya vizuri kwa shule
binafsi, zipo zinazofanya vibaya pia kutokana na wanafunzi wengi kutohudhuria
masomo kwa kukosa ada, gharama kubwa ya masomo. Sababu nyingine amezitaja kuwa
ni uhaba wa walimu kwa baadhi ya masomo, uongozi mbaya na migogoro katika shule
pamoja na mambo mengine.
Akiongelea mikakati ya kuboresha elimu itolewayo nchini, amesema
kuwa serikali imeamua kufanyia marekebisho sera ya elimu na mafunzo ya ufundi
ya mwaka 1995. Amesema kuwa tayari kuna mambo mengi ambayo yamerekebishwa kwa
lengo la kuendana na mahitaji ya utoaji wa elimu bora inayopatikana kwa wote.
Aidha, amewashauri kujenga vyuo vya ualimu na vyuo vingine
ili kukidhi hitaji kubwa la walimu katika shule zote za serikali na binafsi na
wataalamu wengine.
=30=
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni