Alhamisi, 27 Machi 2014

HOTUBA YA MKUU WA MKOA DR. CHRISTINE G. ISHENGOMA WAKATI WA KUFUNGA MAADHIMISHO YA WIKI YA MAJI MKOA WA IRINGA TAREHE 22/ 03/2014 KATIKA KIJIJI CHA IHIMBO WILAYANI KILOLO




Ndugu Katibu Tawala (M),
Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya,
Ndugu Wananchi,
Ndugu Waandishi wa Habari,
Wageni Waalikwa,
Mabibi na Mabwana.
Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Gerald Guninita mbaye ni Mkuu wa Wilaya ya Kilolo

Ndugu Wananchi,
Awali ya yote, napenda kumshukuru Mungu kwa kutujalia afya njema na hatimae leo hii tumekutana hapa.
Aidha, nawashukuru kwa kunialika kuwa mgeni rasmi katika shughuli hii ya leo.
Pia, nitoe shukrani zangu za dhati kwa Kamati ya maandalizi kwa maandalizi mazuri.
Kipekee, navishukuru vikundi vyote vya burudani kwa kutumbuiza vizuri.

Ndugu Wananchi,
Leo ni siku ambayo tunafunga Sherehe za maaadhimisho wiki ya maji. Katika Mkoa wetu wa Iringa, Uzinduzi wa Maadhimisho haya ulifanyika, tarehe 17/03/2014 hapa Ihimbo. Hii ni heshima kubwa mliopewa wananchi wa Ihimbo, naamini heshima hii inatokana na ushirika wenu katika shughuli mbalimbali za maendeleo ikiwemo shughuli za ujenzi wa miradi ya maji. Hivyo nawapongeza sana kwa kujituma kwenu.

Ndugu Wananchi,
Watu wanaopata huduma ya majisafi katika Mkoa wa Iringa ni 441,170 sawa na 63.7% ambapo katika Wilaya ya Kilolo watu 94,288 sawa na 57.9%, Iringa DC watu 172,742 sawa na 68.0% na Mufindi watu 159,763 sawa na 60.1% manispaa watu 116,594 sawa 76.2%. Hali hii bado si nzuri ingawa Tumepiga hatua kubwa na Serikali bado inajipanga kuhakikisha Wananchi Wanapata huduma bora ya maji safi na Salama.

Ndugu Wananchi,
Maadhimisho haya, yanaongozwa na kauli Mbiu. Mwaka huu kauli mbiu ya Wiki ya maji ni Uhakika wa Upatikanaji wa Maji na Nishati. Kaulimbiu hii inatukumbusha changamoto inayotukabili juu ya utunzaji wavyanzo vya maji kama vile Chemchem, Mabwawa, Miito, na Misitu. Utunzaji wa vitu hivi unatuhakikishia upatikanaji wa maji na nishati. Maji na nishati ni vitu vinavyochangamana kwa msingi kwamba maji yanatumika kuzalisha nishati kama vile umeme ambao ni mojawapo ya nishati. Vile vile maji hustawsisha misitu ambayo huzalisha nishati kama vile Mkaa na Kuni. Hivyo basi uhakika wa maji na nishati hutegemea sana utunzaji wa mazingira.

Ndugu Wananchi,
Zipo sheria mbalimbali za utunzaji wa vyanzo vya maji na misitu. Serikali itachukua stahiki kwa mtu au kikundi cha watu pale itakapobainika kwamba sheria ya utunzaji wa mazingira imekiukwa.  Sheria ya Mazingira ya mwaka 2002 unakataza shughuli yoyote ya kibinadamu umbali wa 60m toka ukingo wa mto. Hivyo Wananchi napenda kuwakumbusha juu ya uzingatiaji wa sheria hii muhimu ili tuweze kuepuka  usumbufu wa kuchukuliwa hatua za kisheria lakini vilevile ili tuweze kutunza rasimali maji. Wananchi wa Ihimbo tuwe mfano wa kuigwa na wananchi wa maeneo mengine katika kuhifadhi na kutunza mazingira na vyanzo vya maji kwa ujumla.

Ndugu Wananchi,
Napenda kuchukua fursa hii kusisitiza juu ya kudumisha jumuiya za watumia maji kama chombo cha kutunza miradi ya maji. Pia napenda kuwakumbusha kuwa Serikali imejitoa katika kutunza na kuendesha miradi ya maji, hivyo ni jukumu kuhifadhi na kutunza miundombinu ya maji.

Ndugu Wananchi,
Pamoja na Mafanikio yote tunayopata kupituia Kilimo, tunachangamoto kubwa ya UKIMWI ambao hudhoofisha nguvu kazi na maendeleo kwa ujumla.

Ikumbukwe kwamba  Mkoa wa Iringa kiasi cha Maambukizi ni asilimia 9.1 ambayo bado ni kubwa ukilinganisha na wastani wa maambukizi ya Kitaifa ambayo ni asilimia 5.1%. Tunakazi kubwa ya kufanya kuhakikisha kiasi hiki cha maambukizi kinapungua.

Hivyo, kila mmoja wetu awe mwangalifu na Mkweli lakini pia awe mjumbe katika kupunguza kasi hii ya maambukizi.

Suala la UKIMWI naamini limemgusa kila mmoja wetu kama sio katika familia yake basi Ndugu, Jamaa au marafiki. Vijana ni nguvu kazi ya Taifa, lakini Vijana ndio wapo hatarini zaidi.
 
Viongozi waandamizi wa Mkoa
Ndugu Wananchi,
Suala la Lishe ni Mtambuka na Mkoa Wetu haufanyi vizuri sana ingawa ni wazalishaji wakubwa wa mazao ya Chakula katika Mikoa ya Nyanda za juu Kusini. Tafiti mbalimbali zilizofanyika zinaonyesha kuwa asilimia 52% ya watoto wenye umri chini ya miaka mitano hupata tatizo la udumavu ndani ya Mkoa wetu. Hivyo, tunatatizo kubwa. Naomba tutumie vizuri mazao tunayolima ili kupunguza Tatizo hili. Tule mlo kamili.

Mwisho Ndugu Wananchi,
Naishukuru Serikali kwa kuupa Mkoa wa Iringa Miradi mingi ya Maji ili kuondo Tatizo la Maji kwa Wananchi. Na sisi wananchi tunachotakiwa kuunga Mkono juhudi za Serikali kwa kuhakikisha tunatunza vyanzo vya maji na tunasimamia kikamilifu miradi ya maji.  

MAJI NI UHAI TUYATUNZEASANTENI KWA KUNISIKILIZA

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Habari zinazoendelea hivi sasa

SERIKALI KUWEZESHA VIJANA KUKOPA

Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Iringa Serikali itaendelea kuwawezesha vijana kwa kuwatengenezea mazingira mazuri ya mikopo ili waweze k...