Na. OFISI YA MKUU WA MKOA
SERIKALI
mkoani Iringa imewataka wadau wanaojihusisha na mapambano dhidi ya ukimwi
kuunganisha nguvu zao na kupambana na maambukizi mapya ya virusi vya ukimwi
hasa kwa wanawake na wasichana mkoani Iringa.
Kauli
hiyo imetolewa na Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Wamoja Ayubu alipokuwa
akifungua mkutano wa kujadili matokeo ya utafiti wa hali ya maambukizi ya
virusi vya ukimwi mkoa wa Iringa uliofanyika katika ukumbi wa Wilolesi Hiltop
hoteli mjini Iringa.
Wamoja
amesema “Kwa mujibu wa Utafiti dhidi ya viashiria vya maambukizi ya virusi vya
UKIMWI na Malaria uliofanyika mwaka 2012 unaonesha kuwa maambukizi ya virusi
vya UKIMWI katika Mkoa wa Iringa ni asilimia 9.1 ukiwa unashika nafasi ya pili
nyuma ya Mkoa wa Njombe. Kiwango hiki ni kikubwa kikilinganishwa na wastani wa
maambukizi ya virusi vya UKIMWI kitaifa ambao ni wastani wa asilimia 5.1”.
Amesema kuwa katika mkoa wa
Iringa, wanawake ndilo kundi linalobeba mzigo mkubwa kutokana na tatizo la
maambukizi ya virusi vya ukimwi na ukimwi iliwa kuadhirika zaidi kuliko
wanaume. Amesema kuwa takwimu zinaonesha kuwa wanawake wameathirika kwa
asilimia 11 ikilinganishwa na wanaume ambao wameathirika kwa asilimia 6.9. amesema
kwa mujibu wa takwimu hizo, wanawake ni wahanga kwa asilimia 4.1 zaidi ya
wanaume.
Wamoja amesema kuwa changamoto
hiyo ya kijinsia haijaishia kwa wanawake bali imeendelea hadi katika kundi la
vijana wa kike wenye umri kati ya miaka 15-24. Amesema kundi hilo la wasichana ndiyo wameathirika zaidi na ugonjwa wa
ukimwi ikiwa ni asilimia saba (7) ikilinganishwa na asilimia 1.5 ya wavulana.
Amesema kuwa matokeo ya utafiti huo yatakayojadiliwa siku hiyo yatasaidia
kufafanua tatizo hilo kwa undani na kutoa nafasi pana ya mjadala wa tatizo
husika.
Katibu Tawala Mkoa wa Iringa
amewataka wajumbe wa mkutano huo kujikita katika maeneo ya kimkakati yafuatayo.
Maeneo hayo ameyataja kuwa ni kutambua na kuainisha sababu za kijamii,
kitamaduni na mila zinazochangia katika kuongezeka kwa maambukizi mapya ya
virusi vya ukimwi. Maeneo mengine ni kujipanga kuhakikisha mnayafikia makundi
yaliyo katika hatari kubwa ya kupata maambukizi ya virusi vya ukimwi hasa
wanawake na wasichana wanaofanya kazi za kubadili ngono kwa pesa.
Maeneo mengine ni kuelezea
mipango ya mawasiliano kuhusu mabadiliko ya tabia zenye ufanisi na kuboresha
rufaa pamoja na ushiriki na upimaji wa virusi vya ukimwi, tiba na matunzo kwa
wenye virusi vya ukimwi na ukimwi. Eneo lingine amelitaja kuwa ni upokeaji na
ubora wa huduma ya tohara ya hiari ya kitibabu kwa wanaume kwa lengo la
kujikinga na maambukizi ya virusi vya ukimwi na kupunguza kasi ya kuenea kwa
maambukizi mapya.
Mkutano wa kuwasilisha
taarifa ya utafiti wa kuzuia maambukizi ya virusi vya ukimwi ujulikaoa kama R2P
uliofanyika mjini Iringa umehudhuriwa na wadau mbalimbali wakiwemo watafiti,
wanazuoni na taasisi mbalimbali zikiwemo mpango wa Taifa wa kudhibiti ukimwi,
tume ya taifa ya kudhibiti ukimwi, USAID, REPFAR, kituo cha kudhibiti magonjwa,
idara ya ulinzi, vyuo vikuu vya Johns Hopkins, Tulane na Muhimbili. Taasisi
nyingine ni Jhpiego, AMREF, FHI/360,
PSI, Tunajali, Engender health, Africare, TCCP, JSI na UNICEF.
=30=
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni