Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa 17/3/2014
SERIKALI
mkoani Iringa imejizatiti kusimamia utunzani wa vyanzo vya maji na misitu kwa
kuwachukulia hatua za kisheria wale wote watakaokiuka na kuharibu vyanzo vya
maji.
Kauli
hiyo imetolewa na Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Wamoja Ayubu alipokuwa
akizindua maadhimisho ya wiki ya maji katika mkoa wa iringa katika kijiji cha
Ihimbo wilayani Kilolo.
Wamoja
amesema “serikali itachukua hatua stahiki
kwa mtu au kikundi cha watu pale itakapobainika kwamba sheria ya utunzaji wa
mazingira imekiukwa. Sheria ya mazingira ya mwaka 2002 inakataza shughuli
yoyote ya kibinadamu umbali wa mita 60 kutoka ukingo wa mto”. Amewataka wananchi
kuzingatia sheria hiyo muhimu ili kuweza kuepuka usumbufu wa kuchukuliwa hatua
za kisheria na kuwezesha utunzaji wa rasilimali maji.
Akiongelea
kaulimbiu ya maadhimisho ya wiki ya maji isemayo uhakika wa upatikanaji wa maji
na nishati, amesema kuwa serikali imejipanga vizuri kuhakikisha kaulimbiu
inatekelezwa kwa kulinda sheria mbalimbali za utunzaji wa vyanzo vya maji na misitu.
Amesema kuwa kaulimbiu inakumbusha changamoto inayoukabili mkoa ikiwepo ya utunzaji
wa vyanzo vya maji kama chemchem, mabwawa, mito na misitu.
Amesema
kuwa utunzaji wa rasilimali hizo utauhakikishia mkoa upatikanaji wa maji na
nishati. Amesema kuwa maji na nishati vinategemeana na maji yanatumika kama
vyanzo vya kuzalisha nishati kama mojawapo ya nishati. Ameongeza kuwa maji
hustawisha misitu inayozalisha nishati. Kwa msisitizo amesema kuwa uhakika wa
maji na nishati unategemea sana utunzaji wa mazingira.
Katibu
Tawala Mkoa wa Iringa amewataka wananchi kudumisha jumuiya za watumia maji kama
chombo cha kutunza miradi ya maji. Amesema “napenda
kuwakumbusha kuwa serikali imejitoa katika kutunza na kuendesha miradi ya maji”
amesisitiza Wamoja.
Amesema kuwa ni jukumu la jamii nzima kuunga mkono jumuiya za
maji zinazoundwa katika maeneo yao. Amewataka kutimiza wajibu kwa kutoa
michango inayohitajika na waliyojipangia katika jumuiya zao.
Akiwasilisha
taarifa ya hali ya upatikanaji huduma ya maji katika mkoa wa Iringa kwa mgeni
rasmi katika uzinduzi wa maadhimisho ya wiki ya maji mkoani Iringa, Mhandishi
wa Maji mkoa wa Iringa, Shaban Kitambulio Jellan amesema kuwa
wananchi wanaopata huduma ya maji safi mijini katika mkoa wa Iringa ni 189,644
kati ya wananchi 247,156 ambayo ni sawa na asilimia 76.7 ya wananchi wote
waishio mijini.
Aidha,
hali ya huduma ya maji inategemewa kuongezeka mara baada ya kutekelezwa kwa
miradi katika miji ya Ilula, Kilolo na Mafinga. Amesema kuwa miradi hiyo
inategemewa kutekelezwa kupitia progrmu ya maendeleo ya sekta ya maji (WSDP) na
wananchi wapatao 57,512 wanatarajiwa kupata huduma bora ya maji safi na salama.
Akiongelea
ujenzi wa miradi ya matokeo makubwa sasa (BRN), Mhandishi Jellan amesema kuwa
mkoa unajenga miradi 42 ya maji yenye kuleta matokeo makubwa sasa. Amesema kuwa
miradi hiyo ipo katika hatua mbalimbali za ujenzi. Amesema kuwa mkoa wa Iringa
unahitaji kiasi cha Tshs. Bilioni 11.582 kwa ajili ya kuwalipa makandarasi,
wataalamu waelekezi na usimamizi na ufuatiliaji wa ujenzi wa miradi hiyo.
=30=
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni